Na Saada Almasi, Itilima - Simiyu.
Mkuu wa wilaya ya Itilima mkoani Simiyu Anna Gidarya ametoa agizo kwa halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha hoja za ukaguzi wa mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) zinafanyiwa utekelezaji kwa wakati kwa lengo la kuweka mfumo mzuri wa usimamizi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya wananchi.
Akiwa katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo lililoketi kujadili taarifa ya ukaguzi DC Gidarya amesema kuwa pamoja na kuwa halmashauri hiyo imepata hati safi lakini ni vema kukawa na ufuatiliaji wa karibu wa hoja zilizotolewa na mkaguzi kwani kwa kufanya hivyo uwajibikaji katika matumizi sahihi ya rasilimali za wananchi utaimarishwa.

“Ni lazima tuhakikishe taarifa zote za mali za umma zinaingizwa na kutunzwa katika mfumo wa serikali wa usimamizi wa mali (GAMIS) hii itaongeza uwajibikaji na uwazi pamoja na kuwa tumepata hati safi ni muhimu sasa zile hoja ambazo hazikufikiwa kipindi kilichopita kutekelezwa katika kipindi tulichoingia,” amesema DC Gidarya.
Ameongeza kuwa, “mapungufu yaliyoainishwa na mkaguzi sasa tuyarudie upya ikiwezekana tupate ushauri wa kisheria namna ambavyo tunaweza kwenda sawa na kupata uwiano mzuri wa orodha ya vitu vilivyowekwa katika daftari la kudumu la mali za umma.”

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Itilima, Pendo Kulewa amewataka madiwani halo kuhakikisha miradi ambayo imeanzishwa inatekelezeka kwa muda waliojiwekea na si kuacha viporo ambavyo vinakuja kuwekwa katika mwaka ujao.
“Tuepuke kuanzisha miradi mipya na kuacha miradi viporo ambayo haijakamilika ambayo inakuja kukutana na miradi mipya na pia niagize mapato yote ya ndani ambayo yanapatikana katika halmashauri mzingatie kuyapeleka benki kwa mujibu wa sheria inavyoelekeza,” amesema Pendo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, Daudi Nyalamu pamoja na kukiri kupokea maelekezo ya mkaguzi amewataka madiwani ,wakuu wa idara na watumishi wa wilaya hiyo chini ya mkurugenzi wa halmashauri kuongeza juhudi katika utendaji kazi ili kuhakikisha hakuna hoja za mkaguzi zitakazo jitokeza.
“Mimi nitoe agizo kwa Mkurugenzi wa halmashauri watendaji wapo ni vema upambane nao kwa ukaribu zaidi ili hizi hoja zilizojitokeza awamu hii zisiweze kujitokeza katika awamu tuliyoingia na hiyo miradi ambayo imezungumzwa tuikamilishe kama ilivyokusudiwa,” amesema Nyalamu.

Kwa upande wake Mkaguzi wa ndani mkoa wa Simiyu, Fortunatus Donge amewaambia Madiwani hao kuwa hivi sasa timu ya ukaguzi wa ndani imeanza kufanya maandalizi ya ukaguzi wa mwaka wa fedha 2025/2026 katika halmashauri za mkoa huo hivyo kila halmashauri ijiandae kwa kutoa ushirikiano pale itakapohitajika, ili kufanikisha zoezi hilo kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Discussion
Reader comments
0 contributions