Na Saada Almasi, Maswa - Simiyu.
Mkuu wa wilaya ya Itilima mkoani Simiyu Anna Gidarya ametoa agizo kwa halmashari sita ambazo zinaunda mkoa wa Simiyu kuhakikisha zinatenga maeneo maalum katika kila shule za sekondari ambayo yatakuwa maana viwanja vya michezo ya aina zote tofauti na sasa ambapo shule nyingi zina viwanja vya mpira wa miguu na pete pekee.
Gidaya ametoa agizo hilo wilayani Maswa mkoani humo kwa niaba ya katibu tawala mkoa wa Simiyu wakati wa kilele cha mashindano ya Umoja wa Michezo kwa shule ya za Sekondari Tanzania (UMISETA) yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya wasichana Maswa ambapo katika ngazi ya Halmashauri imeundwa timu ya mkoa ambayo itakwenda kuwakilisha mashindano hayo mkoani Iringa.

“ni vema halmashauri zikashirikiana vizuri na wataalamu wa michezo ili mkapata michoro ya viwanja vitakavyokidhi vigezo vya mashindano mbalimbali maana viwanja vingi tulivyonavyo haviko katika hali nzuri nani kwa mpira wa pete na wa miguu tu wakati michezo tuliyonayo ni mingi na wachezaji wapo,” amesema DC Gidarya.
Ameongeza “vinapokuwepo hivi viwanja ni rahisi hawa kuvizowea mapema siyo inafikia kipindi cha mashandano ndiyo wanaviona hii itasaidia kuongeza ushindani na kuwa na timu bora zaidi kwa mkoa wetu.”

Sambamba na hilo Gidarya amewasisitiza wanafunzi watakaochaguliwa kwenda kushiriki mashindano hayo kuhakikisha wanaidumisha nidhamu kipindi chote cha mashindano.
“kwa ambao mtachaguliwa kushiriki hayo mashindano mkoani Iringa niwaombe kuitunza nidhamu kwa sababu hakuna mafanikio bila nidhamu vilevile mtakapokuwa vizuri kinidhamu mtaupa sifa pia mkoa wetu,” ameongeza DC Gidarya.

Akitoa taarifa ya mashindano hayo Kaimu Afisa elimu mkoa wa Simiyu Erasmus Bureta amesema kuwa matazamio ya kupata timu nzuri ya mkoa ni makubwa kutokana na zaidi ya wanamichezo 800 kushiriki na kuonyesha vipaji vyao.
Katika mashindano hayo halmashauri ya Mji wa Bariadi imeibuka mshindi wa jumla dhidi ya halmashauri tano ambazo zimeshiriki ambazo ni Meatu,Bariadi vijijini, Busega na Maswa.

Discussion
Reader comments
0 contributions