Na Saulo Stephen - Singida.
Katika kuharakisha safari ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuelekea hadhi ya Manispaa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amesema mafanikio ya halmashauri hiyo kufikia hoja za tarakimu moja (Single Digits).
Aidha, hiyo ni pamoja na makusanyo ya mapato zaidi ya asilimia 100 ni ishara kuwa ndoto ya Manyoni kuwa Manispaa inaanza kutimia, huku akisisitiza ubunifu wa kuongeza vyanzo vya mapato, kupunguza madeni na kuongeza kasi ya utekelezaji mara kumi.

Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kujibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Dendego amesema wananchi tayari wameitangulia Serikali katika safari ya kuifanya Manyoni kuwa Manispaa, hivyo kilichobaki ni viongozi na watendaji kutafsiri kwa vitendo vigezo vya maendeleo vinavyohitajika.
Dendego mesisitiza kila robo ya mwaka ipite bila kuzalisha hoja mpya, madeni yalipwe kwa wakati na watendaji waongeze uwepo wao uwandani badala ya kusubiri taarifa maofisini.

"Manyoni kuwa Manispaa inawezekana. Misingi mmeishaijenga; sasa ongezeni ubunifu, mapato na kasi ya utekelezaji mara kumi ili kufikia Dira ya 2050," amesema Dendego.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, ameipongeza Manyoni kwa kufikia Single Digits na kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, huku akitaka halmashauri kuharakisha miradi ya hewa ya ukaa, kuongeza uwekezaji kwenye vyanzo vipya vya mapato na kupunguza madeni ili kupata rasilimali zitakazowezesha maboresho yanayohitajika kuelekea hadhi ya Manispaa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Tano John Makambala, amesema madiwani wamejipanga kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kusimamia miradi ya maendeleo mara kumi zaidi ili kutimiza ndoto ya Manyoni kuwa Manispaa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Anastazia Tutuba, amesema wamepokea maelekezo yote ya viongozi na wamejipanga kuyatekeleza kwa ufanisi.

Manyoni imehitimisha mwaka wa fedha 2025/2026 kwa Hati Safi.
Discussion
Reader comments
0 contributions