Na Daniel Gahu - Katavi.
Kufuatia agizo la Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alilolitoa wakati akihitimisha ziara yake Mkoani Katavi, la kuhakikisha changamoto ya ukosefu wa maji inatatuliwa haraka iwezekanavyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amesisitiza umuhimu wa mipango madhubuti ya huduma ya maji ili kuepusha changamoto zisizo za lazima, akionya uzembe unaoweza kupelekea hali kuwa mbaya kwa wananchi.

Ameyasema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa kwanza wa vyombo vya utoaji huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSOs) uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.
Ambapo katika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama unaimarika katika vijiji vyote na vitongoji vyake, ameiagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), kushirikiana kwa karibu na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ili kupanga na kutekeleza bajeti zinazoakisi mahitaji halisi ya huduma ya maji kwa wananchi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa usimamizi thabiti wa mapato yatokanayo na huduma ya maji, akielekeza kufuatiliwa kwa karibu ankara za matumizi ya maji ili wadaiwa walipe kwa wakati, na pale inapobidi hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaokaidi kulipa.

Sambamba na hilo, amewataka watendaji wa kata na vijiji kuongeza juhudi katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji, akibainisha kuwa usimamizi madhubuti ni msingi wa kudumu wa upatikanaji wa rasilimali hiyo muhimu kwa jamii.
Vilevile, ametoa wito kwa wananchi na viongozi wa kuchaguliwa hususan madiwani kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji kwa kuepuka shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo, akisisitiza kuwa kila mmoja ana wajibu wa kulinda rasilimali hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mzee Kakese Bujiku, mkazi wa kijiji cha Silonge katika Wilaya hiyo ya Tanganyika amesema Serikali ifanikishe kwa haraka mipango ya kuwachimbia kisima katika eneo lao kwani Kwa sasa wanatumia maji ambayo yanatumiwa pia na wanyama jambo ambalo linahatarisha afya zao.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa na mipango mingi na mizuri sana kwa wananchi wa kata yao hasa katika miradi ya maji lakini utekelezaji wake umekuwa ni hafifu sana jambo linalofanya wananchi kuendelea kuteseka na magonjwa ya mlipuko na matumbo hivyo wameiomba Serikali iwasaidie upatikanaji wa huduma muhimu ya maji.



Discussion
Reader comments
0 contributions