Skip to main content

DC APSON ATOLEA UFAFANUZI WA USHURU MAZAO YA ALIZETI

Na Saulo Stephen - Singida.

DC APSON ATOLEA UFAFANUZI WA USHURU MAZAO YA ALIZETI

Na Saulo Stephen - Singida.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson ametoa ufafanuzi juu ya ushuru wa mazao ya Alizeti, akisema hautozwi mara mbili kama inavyodaiwa na baadhi ya Wafanyabiashara, kwani Shilingi 2,000 hulipwa mara moja pekee wakati alizeti ikiwa haijachakatwa inaposafirishwa.

Apson amesema kumekuwa na hoja na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wakidai kuwa wanatozwa ushuru huo mara mbili, hali iliyosababisha mkanganyiko kuhusu utaratibu wa ukusanyaji wa mapato hayo.

"Kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazosimamia ukusanyaji wa ushuru wa mazao, ushuru wa alizeti wa Shilingi 2,000 hutozwa mara moja tu wakati alizeti inaposafirishwa ikiwa bado haijachakatwa," alisema Apson.

Alieleza kuwa baada ya mfanyabiashara kulipa ushuru huo hupewa stakabadhi (risiti) ya malipo ambayo inapaswa kutunzwa kwa kuwa ndiyo uthibitisho rasmi kwamba ushuru umelipwa.

Aidha amesema endapo mafuta yatokanayo na alizeti hiyo yatasafirishwa baada ya uchakataji, mhusika hatapaswa kulipa ushuru huo tena bali atawasilisha risiti ya malipo ya awali kwa mkusanya ushuru kama ushahidi kuwa tayari alishalipa.

"Hivyo basi, si sahihi kudai kuwa ushuru wa alizeti unatozwa mara mbili. Kinachotakiwa ni wafanyabiashara kuhakikisha wanatunza stakabadhi zao za malipo na kuziwasilisha pale zinapohitajika," alisisitiza.

Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, Mkuu huyo wa Wilaya amesema amezielekeza Idara za Biashara pamoja na Maafisa Biashara katika halmashauri zote za wilaya hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu utaratibu wa utozaji wa ushuru ili kuondoa sintofahamu na kuhakikisha sheria zinaeleweka na kutekelezwa ipasavyo.

Amesema utoaji wa elimu hiyo utasaidia kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wafanyabiashara, kuongeza uelewa wa taratibu za ukusanyaji wa mapato na kuondoa malalamiko yasiyo na msingi.

Hata hivyo DC, Apson amewataka wadau wote wa biashara ya alizeti kufuata taratibu zilizowekwa, kutunza nyaraka za malipo na kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha shughuli za biashara zinaendelea kwa ufanisi huku mapato ya serikali yakikusanywa kwa mujibu wa sheria.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.