Skip to main content

COPRA, TBS WAFUNGUA NJIA SOKO LA USHINDANI MAZAO YA WAKULIMA

Wakulima nchini, wameaswa kubadili mtazamo kutoka kulenga wingi wa mazao pekee na kuanza kuzingatia ubora unaokidhi viwango vya soko, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao, kipato cha mkulima na ushindani wa sekta ya kilimo.

COPRA, TBS WAFUNGUA NJIA SOKO LA USHINDANI MAZAO YA WAKULIMA
Studio Narration JAMBO FM

COPRA, TBS WAFUNGUA NJIA SOKO LA USHINDANI MAZAO YA WAKULIMA

0:00 --:--

Wakulima nchini, wameaswa kubadili mtazamo kutoka kulenga wingi wa mazao pekee na kuanza kuzingatia ubora unaokidhi viwango vya soko, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao, kipato cha mkulima na ushindani wa sekta ya kilimo.

Wito huo umetolewa wakati Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walipowakutanisha wadau wa mnyororo wa thamani wa mazao kutoka mikoa ya Katavi, Tabora, Kigoma na Rukwa.

Kikao hicho kimejikita katika kukusanya maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu rasimu za viwango vya kanuni bora za kilimo endelevu pamoja na orodha hakiki za ukaguzi, kwa lengo la kuhakikisha viwango vinavyowekwa vinaendana na mazingira halisi ya uzalishaji na biashara ya mazao.

Kwa mujibu wa Afisa Kilimo Mwandamizi wa COPRA, Bi. Nyandula Mwaijande, ushirikishwaji wa wakulima na wafanyabiashara katika mchakato huo ni muhimu kwa sababu wao ndio wanaokutana moja kwa moja na changamoto za uzalishaji na masoko.

Anasema kuzingatia maoni ya wadau kutasaidia kujenga viwango vinavyotekelezeka na ambavyo vitachochea uzalishaji wa mazao yenye ubora unaokubalika katika masoko yenye ushindani.

Kwa upande wake, Afisa Viwango wa TBS, Sanjo Noel Stephano, amesema uzingatiaji wa viwango unapaswa kuanzia kwenye uzalishaji, utunzaji hadi hatua ya mazao kufikishwa sokoni.

Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuhakikisha mazao ya Tanzania yanakidhi mahitaji ya walaji na kuongeza uwezo wake wa kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa baadhi ya wakulima na wafanyabiashara walioshiriki kikao hicho, hususan wanaojihusisha na zao la mahindi, changamoto imekuwa kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu viwango vinavyotakiwa ili mazao yao yakubalike katika masoko mbalimbali.

Sasa wanasema wamepata uelewa mpya kwamba ubora wa zao unaanzia shambani, na kwamba namna zao linavyolimwa, kuvunwa, kuhifadhiwa na kusafirishwa inaweza kuamua thamani yake sokoni.

Wadau wa kilimo wameipongeza COPRA kwa kuwashirikisha katika mchakato huo, wakisema hatua hiyo inaweza kusaidia kuondoa dhana ya kuzalisha kwa kuangalia wingi pekee na badala yake kujenga utamaduni wa kulima kwa kuzingatia mahitaji ya soko.

Mkulima anayezalisha mazao yenye ubora unaokidhi viwango ana nafasi kubwa ya kupanua masoko, kuongeza thamani ya uzalishaji wake na kupata manufaa zaidi kutokana na kilimo.

Hatua hiyo pia inaweza kuwa kichocheo kwa sekta ya kilimo kwa ujumla, kwani kadiri wakulima wanavyozalisha kwa kuzingatia viwango, ndivyo Tanzania inavyoweza kuongeza ushindani wa mazao yake, kupanua masoko na kuimarisha mnyororo wa thamani kutoka shambani hadi sokoni.

Kwa mantiki hiyo, ujumbe unaotoka katika kikao hiki ni mmoja; mavuno mengi pekee hayatoshi; ubora wa mazao ndio unaoweza kubadili kilimo kuwa biashara yenye tija zaidi kwa mkulima.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.