Na Saulo Stephen - Singida.
Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki, Chief Thomas Mgonto, amewataka wanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Lighwa kutumia muda wao vizuri na kuzingatia masomo ili kufanya vizuri katika mitihani inayowakabili.
Chief Mgonto alitoa rai hiyo alipotembelea Shule ya Sekondari Lighwa, ambapo alipata fursa ya kuzungumza na uongozi wa shule pamoja na wanafunzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu elimu, mazingira ya kujifunzia na maendeleo ya shule.

Katika mazungumzo yake na wanafunzi, aliwahimiza kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuvuruga masomo yao na badala yake kuwa na nidhamu, kujituma na kujiamini ili kufikia malengo waliyojiwekea.
Baada ya ziara hiyo shuleni, Chief Mgonto alikutana na wananchi wa eneo hilo, ambapo alisikiliza kero na maoni yao pamoja na kupokea mapendekezo kuhusu vipaumbele vya maendeleo vinavyohitaji kufanyiwa kazi.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya viongozi na wananchi, kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali na kuharakisha maendeleo ya jamii katika Jimbo la Ikungi Mashariki.

Discussion
Reader comments
0 contributions