Na Ibrahim Rojala - Geita.
Moto ulioelezwa kuwa chanzo chake ni cheche zilizotokea kwenye gari aina ya Canter lenye namba za usajili T 799 BEB lililokuwa limebeba matenki yaliyokuwa yakijazwa mafuta umeteketeza magari mawili na baadhi ya sehemu za kituo cha mafuta, kinachomilikiwa na kampuni ya Lake Energies kilichopo katika eneo la Bombambili, Manispaa ya Geita Mkoani Geita.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo,Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, ASF Keneth Mwakasitu ameeleza kuwa moto huo ulitokea Julai 10, 2026 majira ya saa tano na dakika kumi asubuhi ya kabla ya jeshi hilo kuudhibiti na kufanikiwa kuokoa jengo la utawala,magari matatu,mafuta aina ya Petroli lita 41,000 dizeli lita 40,000 kukiwa hakuna vifo wala majeruhi waliotokana na ajali hiyo.

‘Bado tunataka kufanya uchunguzi kwa kuhusisha taasisi mbalimbali, lakini uchunguzi wa awali umeanzia kwenye gari letu, lakini jeshi limefanikiwa kuudhibiti moto huu,utaona hili ni Cage au ni paa ambalo limeungua, utaona upande wa kule ile dispenser haijamalizika kuungua na utaona jengo la utawala tumeliokoa ni matatizo madogo madogo ya joto yamesababisha vioo kupasuka," ameeleza Mwakasitu.
Kwa upande wa msimamizi wa kituo hicho,Ramadhani Gulamali ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea wakati zoezi la uwekaji wa mafuta ndani ya makontena yaliyokuwa ndani ya gari hilo kabla ya moto kuzuka kwenye betri la gari hilo na kusambaa katika matenki ya mafuta yaliyokuwa ndani ya gari hilo na kusababisha mlipuko ulioplekea moto kuenea katika eneo hilo.

‘Mpaka sasa hivi hasara ni kubwa kwasababu pampu tatu zimeungua zote ikiwemo na kenopi, kwahiyo nadhani miundombinu kwa upande wa pampu nadhani imeharibika yote,kila kitu kimeteketea na moto,’ amebainisha Gulamali.
Nae hudumu wa mafuta katika kituo hicho,Juma Hassan ameeleza kuwa wakati akiendelea kujaza mafuta katika gari hilo ghafla alipewa taarifa kuwa kuna moto nyuma ya gari hilo kabla ya kuchukua kifaa cha kuzima moto ili kukabiliana nao lakini hata hivyo ulimzidi nguvu na kuamua kukimbia.

‘Tulikuwa tunaendelea kuzima na Fire Extinguisher za hapa ofisini kwetu huku tukiendelea kuwasiliana na zimamoto lakini ndio moto ukawa umezidi kuchachamaa ndio ikabidi tukimbie ili kuokoa usalama wetu wa maisha,’ amesema Hassan
Kufuatia tukio hilo,jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Geita ametoa rai kwa wanaobeba mafuta katika magari kuendelea kuchukua tahadhari na kuondokanana tabia za kujiamini kulikopitiliza.


Discussion
Reader comments
0 contributions