Na Ibrahim Rojala - Geita.
Unyanyapaa, upweke, kutoaminiwa na kujengwa kwa dhana potofu ya kuhusika katika vifo vya waume zao vimetajwa kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajane nchini.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa ya wajane walio ndani ya Kanisa la Waadventista Wasabato Katoro Central iliyosomwa na Flora Jeremia Mjalya kwa niaba ya wajane katika ibada maalum ya wajane iliyoandaliwa na Kanisa hilo Mei 23, 2026 ikizitaja changamoto zingine kuwa ni kutokuwa na usaidizi kiuchumi, ugumu katika malezi ya watoto,kutojiamini na kujihisi kupungukiwa.

“Tukio la leo kwetu ni heshima ya pekee tuliyopewa na kanisa na hakika limetuunganisha pamoja na kubadilishana uzoefu wa maisha ya ujane na kututia moyo sisi kwa sisi, tukiendeleza upendo huu miongoni mwetu kwa faida ya maisha ya umilele,” amesema Flora.
Ameeleza kwamba kupitia umoja wao ulionzishwa ndani ya kanisa,wnatarajia kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatembelea wajane na kuwatia moyo, kuwatembelea wagonjwa hospitalini na nyumbani, kuihudumia jamii kupitia huduma za kiroho na misaada kwa watoto wa mitaani na yatima.

Akizungumza kuhusu changamoto zinazowakabili wajane ndani ya jamii,Mjane Leah Kihogo amesema ndani ya baadhi ya jamii wajane wanakabiliwa na changamoto ya kutotambuliwa hivyo kujihisi kuwa wameachwa na jamii na kuwa wapweke akitoa wito kwa jamii kulikumbuka kundi hilo na kuwataka wajane kuwa wavumilivu na kutosita kutafuta misaada ya kisheria na kiroho pale wanapokabiliwa na changmoto mbalimbali.
Naye Mjane Neema Ismail Mayunga ameomba wajane kujengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kutiwa moyo hususani kwa wajane wachanga, akielezea changamoto ya wajane kuonekana ni wanawake wa tofauti waliofanya vitu fulani vilivyosababishwa wanaume wao kufariki mapema hali inayowafanya kushindwa kuishi kwa amani na utulivu.

“Kuna wenzetu wengine wanaachwa wakiwa hawana namna ya kukidhi mahitaji ya familia,watu kama wale kanisa liwabaini liwasaidie kupitia namna yeoyote ile ili maisha yaendelee,” amesema Neema.
Mzee kiongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Katoro Central, Hamis Samson Abdul amesema kanisa hilo lina wajane zaidi ya kumi na kanisa hilo liliona ni vyema kuandaa ibada hiyo maalum kwa lengo la kuwatambua wajane na kuwatia moyo, kuwawezesha kufahamiana na kutiana moyo miongoni mwao.

“Hatutakomea hapo, tutakwenda kwa yatima, watoto wa mitaani ni mnyororo wa huduma hizi katika jamii zinaendela, idara ya vijana imefanya kwa wagonjwa hospitalini na tutaendelea kufanya hivi kulingana na muda na wakati utakavyokuwa ukiruhusu,” ameeleza Mzee Hamis.

Akitoa nasaha kwa wajane ndani ya Kanisa hilo, Mkurugenzi wa wa Majengo wa Jimbo la Nyanza Ukanda wa Dhahabu (NGBF), Mchungaji Godwin Bitwayiki amewataka wajane kutojiona wanyonge na kuwakumbusha kwamba ni Mungu ambaye huamua wa kumtwaa akiwataka kuendelea kusimama imara.
Discussion
Reader comments
0 contributions