Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) Chrispin Chalamila leo June 3, 2026 amewaongoza watumishi wa taasisi hiyo katika mkoa wa Shinyanga kukabidhi mashine mbili za kuhudumia watoto waliozaliwa kabla ya muda katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga mashine ambazo zimenunuliwa kwa michango ya watumishi ili kufanya matendo ya huruma katika jamii.
(TAKUKURU) imekabidhi vifaa tiba hivyo vya kisasa kwa ajili ya kuwahudumia watoto waliozaliwa kabla ya wakati (watoto njiti) katika ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mashine ya kutoa joto kwa watoto wachanga (Radiant Warmer) na mashine ya kutibu ugonjwa wa manjano kwa watoto wachanga (Phototherapy Machine), ambavyo vimenunuliwa kupitia michango ya hiari ya watumishi wa TAKUKURU katika mkoa huo
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Chalamila amesema hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa watumishi wa TAKUKURU katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha huduma za afya nchini.

Amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali na kuboresha miundombinu ya matibabu, jambo ambalo linahitaji kuungwa mkono na wadau mbalimbali ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi.
“Tumeamua kuunga mkono jitihada hizi kwa kununua vifaa tiba kwa ajili ya hospitali mbalimbali nchini. Tayari tumeshatoa vifaa hivi katika mikoa 19, na Shinyanga ni mkoa wa 20. Lengo letu ni kufikia mikoa yote 28 ya Tanzania Bara. Vifaa hivi vimenunuliwa kupitia michango ya hiari ya watumishi wa TAKUKURU,” amesema Chalamila.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. John Luzila, ameishukuru TAKUKURU kwa msaada huo akieleza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza uwezo wa hospitali katika kuwahudumia watoto njiti na wenye uzito mdogo wanaohitaji uangalizi maalum.
Amesema msaada huo wa TAKUKURU unatarajiwa kuongeza uwezo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga katika kutoa huduma bora kwa watoto wachanga, hususan watoto njiti, na hivyo kuchangia kupunguza vifo vya watoto pamoja na kuboresha afya ya mama na mtoto katika mkoa wa Shinyanga.

Dr. Luzila ameeleza kuwa, Mkoa wa Shinyanga unaendelea kukabiliwa na changamoto ya watoto kuzaliwa kabla ya wakati pamoja na watoto wenye uzito pungufu, hali inayoongeza mahitaji ya vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya huduma za watoto wachanga.
Amebainisha kuwa kwa mujibu wa takwimu za miezi mitatu iliyopita, hospitali hiyo imepokea watoto kadhaa wenye uzito pungufu na waliozaliwa kabla ya wakati, ambapo wengi wao wamefanikiwa kupata matibabu na kurejea katika maisha ya kawaida kutokana na huduma zinazotolewa hospitalini hapo.

Dr. Luzila pia ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha wadau mbalimbali kushiriki katika kuboresha huduma za afya, huku akitoa mwaliko kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia sekta hiyo muhimu.
Naye mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amesema taasisi hiyo katika mkoa huo imekuwa na mahusiano mazuri katika kufanya kazi na na kwamba wameshaendesha semina mbalimbali katika kuwajengea uelewa watumishi katika hospitali hiyo juu ya maadili na mapambano dhidi ya rushwa katika jamii na kuhaidi kuendelea kushikamana ili kujenga jamii madhubuti.

Kessy ameupongeza pia uongozi katika hospitali hiyo kwani miradi mingi ya seriakli imesimamiwa kwa weledi na kuanisha jumla la semina namafunzo ambayo kama taasisi wameyatoa hospitalini hapo.
Aidha Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto katika hospital hiyo Dr Yustiana Tizeba amesema vifaa hivyo vimewafikia kwa wakati muafaka kwani yalikuwa ni mahitaji makubwa kwa sasa katika huku akiwataka wadau wengine kujitokeza kusaidia itengi hicho cha watoto waliozaliwa kabla ya muda.

Watoto waliozaliwa kabla ya muda ni pale mzazi anapojifungua kabla ya kutimiza wiki 37 za ujauzito na baadhi ya viungo vyao kama mapafu, mfumo wa kinga na mfumo wa mmeng'enyo wa chakula huwa havijakomaa kikamilifu. Hali hii huwafanya wahitaji uangalizi maalumu ikiwemo kutumia mashine hizo ili kuhakikisha wanakua na kuwa na afya njema.
Discussion
Reader comments
0 contributions