Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limeonya vikali dhidi ya vitendo vya Chagulaga vinavyodaiwa kuwaweka katika mazingira ya hofu na hatari wasichana wadogo, likisisitiza kuwa watu watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria na kufungwa hadi miaka 30 jela.
Onyo hilo limetolewa katika Kata ya Ilunde, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele, wakati wa mwendelezo wa programu ya “Ongea na Kamanda” inayolenga kuwapa wananchi nafasi ya kueleza changamoto za kiusalama na kupata ufumbuzi kutoka kwa Jeshi la Polisi.

Katika mkutano huo, wananchi wameiibua changamoto ya Chagulaga, wakieleza kuwa vitendo hivyo vimeendelea kuleta hofu kwa watoto, hususan wasichana wadogo, jambo lililolifanya Jeshi la Polisi kutoa tahadhari kwa jamii na kuwataka wananchi kutoa taarifa mapema.
Kamanda wa Polisi Jamii Mkoa wa Katavi, John Mwaipungu, amewataka watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kuviacha mara moja, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi linachukulia suala hilo kwa uzito kutokana na athari zake kwa usalama na ustawi wa watoto.

Mwaipungu pia amewataka wazazi kuimarisha malezi bila ubaguzi wa kijinsia, kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume wanapatiwa ulinzi, elimu na mwongozo unaowawezesha kujitambua na kuepuka mazingira yanayoweza kuhatarisha usalama na mustakabali wao.
Mkazi wa Kata ya Ilunde, Kijiji cha Ibela Mafipa, Masanja Magadula, amesema baadhi ya wasichana wadogo wamekuwa wakiishi kwa hofu wanapopita katika maeneo yao kutokana na hofu ya kukutana na baadhi ya vijana wanaodaiwa kujihusisha na vitendo hivyo.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Katavi, ACP Inongu Kimasa, amewataka wanaume wanaofanyiwa ukatili majumbani, ikiwemo kupigwa na wake zao, kutonyamaza bali kutoa taarifa katika Dawati la Jinsia na Watoto la Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mkutano huo pia umeibua changamoto nyingine zinazowakabili wananchi wa Ilunde, ikiwemo migogoro ya maeneo ya kilimo na malisho pamoja na malalamiko ya baadhi ya wananchi kufukuzwa katika mashamba wanayodai kuwa Serikali imeyatambua kuwa maeneo ya hifadhi, huku Jeshi la Polisi likiahidi kufikisha changamoto hizo katika mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Kwa ujumla, Jeshi la Polisi limewataka wananchi wa Ilunde na Katavi kwa ujumla kutokaa kimya wanapobaini vitendo vinavyohatarisha usalama wa watoto, wanawake au wanaume, likisisitiza kuwa taarifa za mapema zinaweza kusaidia kuzuia uhalifu, kulinda waathirika na kuhakikisha wanaokiuka sheria wanachukuliwa hatua.
Discussion
Reader comments
0 contributions