Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kutembelea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kwenye Kata hiyo ikigusa sekta ya Elimu, Afya, Maji na uuzwaji wa pamba kwenye baadhi ya Amcos ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa ufanisi na wananchi wanapata huduma bora huku utekelezaji wa maagizo ya serikali ukitekelezwa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Kishapu, Joel Ndettoson amesema, Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika kuboresha miundombinu ya huduma za jamii, hatua inayochochea maendeleo ya wananchi na kuboresha maisha yao.

Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa choo cha kisasa Ujenzi wa choo cha kisasa katika eneo la maegesho ya magari ya lililopo katika mnada wa Mhunze ulioko Kitongoji cha Mwasele "B" chenye jumla ya matundu matatu (3) pamoja na chumba cha mkusanya mapato pamoja na Ujenzi wa matundu matano ya vyoo katika Shule ya Msingi Lubaga.
Miradi mingine ni Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Serikali, ukiwa ni mfano wa ushirikiano utakaoleta matokeo makubwa shule ya msingi Mwabusiga na Mradi wa tanki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 50,000 litakalohudumia wananchi wa Mwabusiga pamoja na Mradi mkubwa wa BOOST katika Shule ya Sekondari Isoso.

Kamati pia ilikagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi ndani ya Shule ya Sekondari Isoso unaotekelezwa kupitia fedha za Serikali Kuu chini ya Programu ya BOOST ambapo Mradi huo ulipokea jumla ya Shilingi 342,900,000 kwa ajili ya kujenga Vyumba sita vya madarasa ya shule ya msingi, Matundu 10 ya vyoo vya shule ya msingi, Vyumba viwili vya madarasa ya awali, Matundu sita ya vyoo vya shule ya awali, Jengo la utawala na Matundu mawili ya vyoo vya walimu.
Kazi za ujenzi zilianza rasmi Septemba 1, 2025 na kufikia Juni 30, 2026 miundombinu yote iliyopangwa ilikuwa imekamilika kwa asilimia 100 kupitia mfumo wa Force Account chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu huku jumla ya Shilingi 340,995,000 zikiwa tayari zimetumika, na salio la Shilingi 1,905,000 likisubiri kulipwa kama retention baada ya kukamilika kwa taratibu za uthibitishaji wa kazi.

Aidha, kamati hiyo pia imekagua Mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Isoso uliogharimu Shilingi 71,800,000 kupitia Programu ya BOOST huku ikielezwa kuwa Fedha hizo zilitumika kununua vifaa vya ujenzi, kugharamia nguvu kazi na matumizi mengine ya ujenzi.
Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umeanza kutumika, ambapo wanafunzi 97 wa elimu ya awali wameanza kutumia madarasa hayo tangu Aprili 2026.

Mbali na hivyo kamati hiyo ya siasa imetembelea na kufanya ukaguzi katika AMCOS ya Lubaga na Buluba Mhunze tawi la Mwabusiga ili kujionea hali halisi ya ununuzi na uuzaji wa zao la pamba ambapo wananchi wameonesha kuridhishwa na malipo kuwa ya haraka na papo kwa papo ikilinganishwa na msimu uliopita na kwamba kwasasa malipo yanafanyika kwa njia ya kidijitali jambo lililokuwa likichelewesha malipo yao na kungeza migogoro kwenye zao hilo.
Kamati hiyo pia imetembelea Zahanati ya Lubaga, ambapo Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Christian Ngowi ameelezea mapungufu yaliyopo huku viongozi wa Chama ahicho na Diwani wa Kata wakiahidi kuzifikisha mahali husika ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi.

Baada ya kukagua miradi yote, Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Kishapu imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo na kuipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya wananchi na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa usimamizi makini.
Pia Kamati imeshauri kuwepo na marekebisho kwenye baadhi ya miradi kwenye nyufa zilizoonekana kabla ya mradi kukabidhiwa huku wakiwataka wananchi kuendelea kushiriki katika ulinzi na utunzaji wa miradi hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Discussion
Reader comments
0 contributions