Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Nazir Karamagi, imeridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Manispaa ya Bukoba, ikiwemo mradi wa ujenzi wa soko kubwa la kisasa wenye thamani ya shilingi bilioni 18.
Soko hilo linatarajiwa kuwa kitovu kikuu cha shughuli za biashara katika Manispaa ya Bukoba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla, huku likitarajiwa kuongeza fursa za ajira, kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia shughuli za kiuchumi.

Mbali na mradi huo, Kamati ya Siasa ilikagua pia ujenzi wa jengo jipya la Manispaa ya Bukoba pamoja na mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, ambayo inalenga kuboresha huduma za afya na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Dkt. Nazir Karamagi, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.

Alisema miradi hiyo ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya huduma, kuboresha ustawi wa jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kagera.
Aidha, aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora, kukamilisha kazi kwa wakati na kutumia ipasavyo fedha za umma ili wananchi waanze kunufaika na uwekezaji huo bila kuchelewa.

Nao, baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba wameeleza matarajio makubwa ya kunufaika na kukamilika kwa miradi hiyo, hususan soko la kisasa ambalo linatarajiwa kuondoa changamoto za mazingira ya biashara, kuongeza fursa za ajira, kuvutia wawekezaji na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.

Discussion
Reader comments
0 contributions