Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro, ametoa wito kwa wafanyabiashara kutoka nchi jirani za DR Congo na Burundi kuwekeza Mkoani humo kutokana na uwepo fursa nyingi za uwekezaji katika Sekta za viwanda, biashara, Uchukuzi, Kilimo, Uvuvi na Utalii.
Balozi Sirro ametoa wito huo wakati akifungua rasmi maonesho ya biashara ya Lake Tanganyika International Expro 2026, yaliyofanyika Manispaa ya Kigoma Ujiji na kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka nchi za Burundi, DR Congo na Mikoa mbalimbali nchini.

Amesema maonesho hayo yameonesha mafanikio kwa kuunganisha wazalishaji wa bidhaa na masoko pamoja na kuvutia wawekezaji na wabia wa Maendeleo sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia, kuibua ubinifu na kukuza biashara, ajira na uchumi wa wananchi.
Aidha, Sirro alisisitiza kuwa maonesho hayo yanalenga kuimarisha diplomasia ya uchumi katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa lengo la kukuza uchumi wa mataifa hayo kupitia mafanikio ya mtu mmoja mmoja au taasisi.
Waziri wa Madini Mkoa wa Tanganyika nchini DR Congo Mateka Simplis, amesema uhusiano unazidi kuimarika katika sekta ya biashara baina ya nchi hiyo na Tanzania unatoa fursa muhimu ya kuzifungua pande mbili hizo kiuchumi.
Amesema nchi hiyo imekuwa ikitegemea bidhaa nyingi kutoka Tanzania ambapo amewasisitiza wafanyabiashara nchini kuendelea kushirikiana kwa karibu na wenzao wa Congo ili kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa pande zote mbili.
Mwakilishi wa Balozi katika Ubalozi mdogo wa DR Congo, Adalbert Nininahazwe amesema maonesho ya Lake Tanganyika International Expro 2026 yanapaswa kuwa endelevu huku yakionesha ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na kimahusiano baina ya nchi shiriki.
Maonesho ya Lake Tanganyika International Expo 2026 yameandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na Chemba ya wafanyabiashara (TNCC) na kudhaminiwa na Program ya Pamoja ya Kigoma (KJP), Shirika la Enable pamoja na Mati Super Brand Co. Ltd.
Discussion
Reader comments
0 contributions