Na Saulo Stephen - Singida.
Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Makwasa Bulenga, ameendelea kusisitiza umuhimu wa lishe bora shuleni kwa vitendo, akieleza kuwa mpango huo unachangia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi na kuwafanya washiriki kikamilifu katika masomo.
Bulenga alitoa kauli hiyo alipokuwa akitembelea Shule ya Msingi Kikhonda iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, ambapo alipata fursa ya kujionea utekelezaji wa programu ya lishe shuleni na kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi.

Amesema lishe bora huwapa wanafunzi nguvu na uwezo mzuri wa kufikiri, jambo linaloboresha mchakato wa kujifunza, kuongeza umakini darasani na hatimaye kuinua kiwango cha ufaulu.
Aidha, amehimiza shule zote kuendelea kuimarisha programu za lishe kwa kushirikiana na wazazi, jamii na wadau wa elimu, akisisitiza kuwa uwekezaji katika lishe ni msingi muhimu wa maendeleo ya elimu na ustawi wa mwanafunzi.

Bulenga amebainisha kuwa utoaji wa lishe shuleni si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa pamoja unaohitaji ushirikiano wa wadau wote ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia na kufikia ndoto zake.
Discussion
Reader comments
0 contributions