Na Clavery Christian Bukoba - Kagera.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba imeadhimisha Wiki ya Maabara Nchini kwa kutoa huduma za vipimo pamoja na elimu ya huduma za maabara bure kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya mapema.
Akisoma risala kwa niaba ya Idara ya Maabara, Meneja wa Maabara wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Eustadius Kamugisha amesema kuwa vipimo vinavyotolewa bure ni pamoja na vipimo vya magonjwa ya ini na figo, saratani ya mlango wa kizazi, malaria, VVU, tezi dume, sukari, makundi ya damu, pamoja na kipimo cha uzito na shinikizo la damu.

Alieleza kuwa Idara ya Maabara imepiga hatua kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ubora na kuingia katika hatua mbalimbali za ukuaji na maendeleo ya kitaaluma.
Bwana Kamugisha alisema kuwa mwaka 2015 maabara hiyo ilipata nyota moja ya ubora, mwaka 2018 ilipata nyota tatu kupitia ukaguzi wa Wizara ya Afya, na mwaka 2022 ilifanikiwa kupata ithibati ya kimataifa kutoka SADCAS, taasisi ya ithibati chini ya SADC.

Naye, Mratibu wa Huduma za Maabara Mkoa wa Kagera, Emmanuel Mkumbo, amesema kuwa hospitali hiyo imeendelea kupanua wigo wa huduma za maabara kutoka huduma chache hadi kufikia zaidi ya vipimo 100 kwa sasa.
Aliongeza kuwa ongezeko la wataalamu wa maabara na uboreshaji wa miundombinu ni matokeo ya jitihada za serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za kisasa.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Salum Kimbari alisema, huduma za vipimo bure zitaendelea kutolewa kuanzia tarehe 20 Aprili 2026 hadi Ijumaa tarehe 24 Aprili 2026, na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa afya zao.
Discussion
Reader comments
0 contributions