Na Clavery Christian, Muleba - Kagera.
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Adonis Bitegeko, amekabidhi sare 110 za shule kwa wanafunzi wa shule nne za msingi zilizopo jimboni humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji na kuongeza motisha ya kujifunza.
Bitegeko alikabidhi sare hizo, wakati wa ziara yake katika Shule za Msingi Rwakahoza, Kabuleme, Omkyaya na Kashumbililo. Katika ziara hiyo aliambatana na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi wa Serikali kutoka sekta ya elimu.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bitegeko alisema lengo la msaada huo ni kupunguza mzigo wa gharama za sare kwa wazazi wenye uwezo mdogo wa kifedha na kuwasaidia watoto yatima ili wapate fursa ya kusoma katika mazingira bora, yenye heshima na kujiamini.
Mbali na kukabidhi sare hizo, mbunge huyo alifanya vikao vya ndani na walimu wa shule hizo, ambapo walijadili mikakati ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji, kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazokabili shule hizo.

Pia aliwataka wazazi na walezi kuongeza ushirikiano katika malezi ya watoto kwa kuhakikisha wanahudhuria masomo kila siku na wanapata mazingira bora ya kujifunza ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu.
Pia mbunge huyo aliahidi kuendelea kushirikiana na wananchi kutatua changamoto zinazoikabili Muleba Kaskazini, akitaja maeneo ya elimu, huduma za maji, umeme, afya na miundombinu ya barabara kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake vya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wote wa jimbo hilo.




Discussion
Reader comments
0 contributions