Wananchi mkoani Kagera wameishukuru serikali kwa kuwapatia bima ya afya, wakieleza kuwa hatua hiyo imewasaidia zaidi wananchi wenye kipato cha chini ambao awali walishindwa kwenda vituo vya afya kupata matibabu na kulazimika kubaki nyumbani bila huduma za matibabu.
Wamesema bima ya afya ina mchango mkubwa katika kupunguza gharama za matibabu, hasa kwa wananchi wenye uchumi mdogo ambao hukabiliwa na changamoto ya kumudu gharama kubwa za matibabu wanapopatwa na magonjwa.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Yahya Ramadhani Kido, amesisitiza vitengo mbalimbali, ikiwemo Bohari ya Dawa, kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote ili kuepusha changamoto ya wananchi kukosa huduma wanapofika katika zahanati na vituo vya afya.
Aidha, Kido amewataka viongozi kuhakikisha bima ya afya inakuwa ajenda ya kudumu katika vikao vyao ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi kujiunga na bima ya afya kwa wote, ambayo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi, hususan wenye kipato cha chini.

Bima ya afya kwa wote ni utaratibu uliowekwa na serikali unaolenga kuhakikisha kila raia wa Tanzania anapata uhakika wa huduma za matibabu kwa gharama anazoweza kumudu.
Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Ismail Kangenta, amesema wananchi wasio na uwezo wa kulipia bima wametambuliwa na serikali imewalipia, huku wenye uwezo wakitarajiwa kuanza kulipia bima ya Fahari kwa gharama ya shilingi 150,000 kwa familia yenye watu sita.

Kangenta amesema mpaka Sasa muitikio wa wananchi ni mkubwa lakini pia bima hiyo inawawezesha mwanachama kupata huduma za msingi za matibabu kuanzia ngazi ya zahanati, kituo cha afya hadi ngazi ya rufaa, kulingana na huduma zinazotolewa katika mpango huo.

Ameongeza kuwa ushirikishwaji katika awamu hii ni mkubwa, ukihusisha viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi kitongoji, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, elimu ya kutosha na hamasa ya kuendelea kujisajili ili kufanikisha upatikanaji wa bima ya afya kwa wote.
Discussion
Reader comments
0 contributions