Skip to main content

BILIONI 29 ZAPATIKANA KUPITIA UHIFADHI WA MISITU TANGANYIKA

Na Daniel Gahu - Katavi.

BILIONI 29 ZAPATIKANA KUPITIA UHIFADHI WA MISITU TANGANYIKA

Na Daniel Gahu - Katavi.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imeendelea kujijengea heshima na kutambulika kitaifa kama kitovu cha mafunzo ya biashara ya kaboni baada ya kupokea viongozi na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Makete waliowasili kujifunza mbinu bora za utekelezaji wa biashara hiyo.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za halmashauri mbalimbali nchini kujifunza namna Tanganyika ilivyofanikiwa kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi kupitia biashara ya kaboni. Hadi sasa, zaidi ya halmashauri 50 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania zimefika wilayani humo kupata uzoefu kuhusu usimamizi wa biashara ya kaboni, uhifadhi wa misitu na matumizi ya mapato yatokanayo na shughuli hiyo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Shabani J. Juma, amesema mafanikio yaliyofikiwa na halmashauri hiyo yameifanya kuwa mfano wa kuigwa nchini katika utekelezaji wa biashara ya kaboni.

Ameeleza kuwa kupitia uhifadhi wa misitu katika vijiji nane vinavyoshiriki mpango huo, halmashauri imefanikiwa kupata zaidi ya shilingi bilioni 29 tangu kuanza kwa biashara ya kaboni. Fedha hizo zimekuwa chachu ya maendeleo kwa jamii kwa kuelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, sehemu ya fedha hizo imetumika kuboresha huduma za afya kwa kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma, kuboresha sekta ya elimu kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule pamoja na kugharamia huduma nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi wa vijiji vinavyoshiriki mpango huo.

Ndg. Shabani Juma amesema mafanikio hayo yameongeza hamasa kwa halmashauri kuendelea kupanua wigo wa biashara ya kaboni kwa kuingiza maeneo mapya ya misitu yenye uwezo wa kuzalisha mikopo ya kaboni.

Amebainisha kuwa hatua inayofuata ni kuhusisha Misitu ya Tongwe Mashariki na Tongwe Magharibi katika mpango huo, hatua ambayo inalenga kuongeza mapato ya wananchi, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuhakikisha rasilimali za misitu zinaendelea kuwa chanzo endelevu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanganyika, Ndg. Alison Uisso, amesema mafanikio hayo hayakupatikana kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya usimamizi madhubuti wa rasilimali za misitu pamoja na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya uhifadhi.

Amesema serikali itaendelea kuimarisha doria za misitu, kusimamia sheria za uhifadhi na kuendelea kuwashirikisha wananchi katika kulinda mazingira ili kuhakikisha misitu inaendelea kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Katibu Tarafa wa Tarafa ya Ikuwo, Wilaya ya Makete, Ndg. Albert Luwondo, aliyewakilisha wataalamu walioshiriki mafunzo hayo, amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kwa kuwapatia elimu ya kina pamoja na uzoefu wa vitendo kuhusu biashara ya kaboni.

Amesema maarifa waliyoyapata yatawasaidia kuboresha usimamizi wa misitu katika Wilaya ya Makete, kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi na kutumia biashara ya kaboni kama fursa ya kuongeza mapato na kuleta maendeleo endelevu katika maeneo yao.

Kuendelea kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika kupokea viongozi na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali nchini ni uthibitisho kuwa biashara ya kaboni imekuwa moja ya nyenzo muhimu zinazounganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya wananchi. Mafanikio hayo yanaifanya Tanganyika kuwa mfano wa kitaifa katika matumizi endelevu ya rasilimali za misitu, huku yakitoa dira kwa halmashauri nyingine zinazotaka kunufaika na fursa ya uchumi wa kaboni.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.