Na Clavery Christian, Bukoba - Kagera.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera imeteketeza takribani tani 30 za bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kwa njia ya magendo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali za kulinda afya za wananchi, mazingira na uchumi wa taifa dhidi ya bidhaa zisizokidhi viwango na taratibu za kisheria.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Kaimu Meneja wa Forodha wa TRA Mkoa wa Kagera, Amos Katushabe, alisema bidhaa hizo zilikamatwa kupitia operesheni maalumu zilizofanyika kwa ushirikiano kati ya TRA, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taarifa kutoka kwa wananchi.

Alisema ushirikiano huo umewezesha kuzuia bidhaa hizo kuingia sokoni, hatua ambayo imeepusha madhara makubwa ambayo yangeweza kuwakumba watumiaji pamoja na kuathiri mapato ya serikali.
"Bidhaa hizi zilinaswa kupitia taarifa za wananchi na operesheni za pamoja. Lengo letu ni kuhakikisha bidhaa zisizo halali haziingii sokoni na kuhatarisha afya za wananchi wala kudhoofisha uchumi wa nchi," amesema Katushabe.

Alibainisha kuwa bidhaa zilizoteketezwa ni pamoja na pombe haramu, sigara, vyakula vilivyokwisha muda wa matumizi, vipodozi vilivyopigwa marufuku na serikali, pamoja na dawa za binadamu na wanyama ambazo hazikukidhi matakwa ya sheria na viwango vinavyotakiwa.
Afisa Mdhibiti Ubora wa Kanda ya Ziwa Magharibi kutoka Wakala wa Viwango Tanzania (TBS), Vicent Mabura, aliwataka wananchi kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa mbalimbali kwa kuhakikisha zinakuwa na alama ya ubora ya TBS pamoja na muda sahihi wa matumizi.

Mabura alisema tahadhari hiyo itasaidia kulinda afya za watumiaji na kupunguza matumizi ya bidhaa zisizo salama ambazo zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa jamii.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini uwepo wa bidhaa zinazohisiwa kuingizwa kwa njia ya magendo au zisizokidhi viwango, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.


Discussion
Reader comments
0 contributions