Katika Mkoa wa Kagera, jumla ya kaya 38,217 zenye wanufaika 84,934 zinatarajiwa kusajiliwa katika awamu ya pili ya mpango wa Serikali wa Bima ya Afya kwa Wote, wenye lengo la kupunguza changamoto za wananchi kupata huduma za matibabu.
Akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa huo, Yahaya Ramadhani Kido, amesema mpango huo unahusisha kaya zinazolipiwa na Serikali pamoja na makundi mengine ya wanachama, vikundi vya kijamii na vyama vya ushirika.

Amesema kuanzishwa kwa mpango huo kutasaidia kuboresha ustawi wa wananchi kwa kupunguza gharama za matibabu na kuwawezesha kupata huduma za afya wanapozihitaji.
Katika awamu ya kwanza, Serikali ililipia kaya 15,284 zenye wanufaika 67,451, huku utekelezaji wa usajili ukifikia asilimia 79 ya lengo lililowekwa, ikilinganishwa na lengo la kitaifa la asilimia 80.

Hata hivyo, Manispaa ya Bukoba pamoja na Halmashauri za Missenyi na Karagwe zimetajwa kuwa zimeandikisha wanufaika zaidi ya lengo la kitaifa, ikilinganishwa na halmashauri nyingine za Mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake, Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Kagera, Ismail Kangeta, amesema watahakikisha kaya zenye hali duni ya kiuchumi zinapata huduma za afya kupitia mpango huo. Ameeleza kuwa hadi wakati wa uzinduzi, kaya 38,217 zilikuwa zimesajiliwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi na umuhimu wa bima ya afya.

Kangeta amesisitiza pia haja ya kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi kujiunga na bima hiyo ili kuongeza idadi ya wanufaika wanaofikiwa na mpango huo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kujiunga na bima ya afya ili kupata uhakika wa huduma za matibabu, huku akiwaelekeza viongozi na uongozi wa NHIF kusimamia upatikanaji wa huduma bora na kwa wakati kwa wanachama, hatua inayolenga kuongeza imani katika mpango huo.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kata ya Kashai, Manispaa ya Bukoba, wameomba kuendelea kupewa elimu kuhusu magonjwa yanayotibiwa na bima ya shilingi 150,000 ili kuondoa usumbufu wakati wa kupata huduma. Wamesema kujiunga na bima hiyo ni muhimu, hasa kwa familia zenye kipato cha chini, kwa kuwa kutawasaidia kupata huduma za afya bila kukabiliwa na gharama kubwa za matibabu.

Discussion
Reader comments
0 contributions