Na Ibrahim Rojala - Geita.
Jumla ya watoto 1,114,918 wenye umri chini ya miaka 10 mkoani Geita wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya matone ya Polio mkoani Geita kupitia awamu ya kwanza ya utekelezajiwa kampeni ya chanjo hiyo ambayo awamuya kwanza ya utekelezaji wake inatarajiwa kufanyika kati ya Machi 24 hadi Machi 27, 2026.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt.Omary Sukari ameeleza hayo Machi 19, 2026 ambapo amebainisha kwamba maandalizi ya chanjo hiyo yamekamilika ikiwa ni pamoja na watumishi wa Afya zaidi ya 6000 waliojengewa uwezo,walio tayari kwa utoaji wa huduma na dozi za chanjo.

Aidha amebainisha kuwa dozi za chanjo zipatazo 1,300,000 zimepokelewa na kufikishwa katika vituo vya huduma,pamoja na uwepo wa watoa huduma ngazi ya jamii ambao pia wamepatiwa mafunzo na kueleza kuwa chanjo hizo ni salama zisizo na madhara ya aina yoyote.
"Kama mnavyofahamu,dunia sasa hivi ipo kwenye hatua za mwisho za kuondosha ugonjwa wa Polio duniani,lakini bado zipo nchi ambazo zina visa vya ugonjwa wa polio na ndani ya nchi yetu kwa muda mrefu tulikuwa hatuna hivi visa, ili kuuondosha kabisa njia pekee ni kuhakikisha watoto wetu wanapata chanjo,wanakingwa dhidi ya ugonjwa wa polio," amesema Dkt. Sukari
Mratibu wa Elimu ya afya kwa Umma mkoa wa Geita, Pascazia Benard Madulu amewaomba wananchi kuonesha ushirikiano kwa kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo hiyo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa polio ambao miongoni mwa madhara yake ni pamoja na kusababisha ulemavu wa kudumu.

Akizungumzia uamuzi wa utekelezaji wa zoezi la utolewaji wa chanjo hiyo, Afisa Programmu wa Mpango wa Taifa wa chanjo kutoka Wizara ya Afya, Michael Ndowa ameeleza kuwa kampeni ya chanjo ya matone ya Polio inatarajiwa kutolewa katika mikoa saba inyouzunguka mkoa wa Mwanza.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Mwanza, Mara, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Singida na Geita, akieleza kuwa inatarajiwa kutolewa kwa zaidi ya watoto milioni sita katika mikoa hiyo walio na umri chini ya miaka kumi (10).
Hatua ya utolewaji wa chanjo hiyo imekuja kufuatia matokeo ya ufuatiliaji yaliyofanywa na Wizara ya Afya kubaini uwepo wa kiashiria cha kirusi cha polio kutoka katika moja kati ya Sampuli iliyopimwa mkoani Mwanza hali iliyoilazimu wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI, Shirika la Afya duniani (WHO), kuja na mpango wa kuwakinga watoto wote walio na umri chini ya miaka 10 dhidi ya ugonjwa wa polio.

"Na hii kampeni ambayo tutaifanya kuanzia tarehe 24 mpaka 27 kwa awamu ya kwanza katika hii mikoa yote,lakini kwa awamu ya pili,tutafanya kuanzia tarehe 7 mpaka tarehe 10,mwezi wa tano, dhumuni kubwa likiwa ni kuwakinga hawa watoto dhidi ya kirusi cha polio,tunasema tukifanya mazoezi haya kwa awamu mbili tutakuwa tumetengeneza kinga madhubuti kwaajili ya kuwahikishia watoto wamekingwa dhidi ya Polio," amesema Ndowa.
Kwa ujumla kampeni ya chanjo ya Polio inafanyika kwa lengo la kuimarisha kinga kwa jamii, kuzuia maambukizi ya virusi vya Polio kuenea kwa jamii, kuwakinga watoto dhidi ya ulemavu wa kudumu na madhara mengine ya ugonjwa wa Polio.
Aidha inafanyika katika kipindi ambachohakuna mtoto aliyethibitika kuugua ugonjwa wa Polio nchini Tanzania, hivyo kampeni hii inafanyika kama hatua za tahadhari za kuwakinga watoto na jamii kwa ujumla wasipate maambukizi ya ugonjwa wa Polio ambaokisa cha mwisho chakuripotiwauwepowake ilikuwa ni mnamo Julai 1996.
Discussion
Reader comments
0 contributions