Skip to main content

ASKOFU NYAISONGA AZINDUA KLINIKI YA MACHO KASULU

Rais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (AMECEA) na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga, amezindua huduma za kibingwa za kliniki ya macho pamoja na jengo jipya la kutolea huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu, mkoani Kigoma.

ASKOFU NYAISONGA AZINDUA KLINIKI YA MACHO KASULU
Studio Narration JAMBO FM

ASKOFU NYAISONGA AZINDUA KLINIKI YA MACHO KASULU

0:00 --:--

Rais wa Mabaraza ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki katika Ukanda wa Mashariki mwa Afrika (AMECEA) na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga, amezindua huduma za kibingwa za kliniki ya macho pamoja na jengo jipya la kutolea huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga, iliyopo Halmashauri ya Mji wa Kasulu, mkoani Kigoma.

Akizungumza akiwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi huo, Askofu Mkuu Nyaisonga amesisitiza umuhimu wa kutunza na kulinda miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wenye changamoto za magonjwa ya macho.

Muonekano wa jengo lililozinduliwa kwa ajili ya utoaji wa huduma za macho, Picha na Tryphone Odace

“Ni muhimu kuhakikisha miundombinu hii inatunzwa vizuri ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wanaohitaji matibabu ya magonjwa ya macho,” alisisitiza Askofu Nyaisonga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, alisema kuanzishwa kwa huduma hizo kutasaidia kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi wa Kigoma na maeneo jirani.

Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Luteni Kanali Joseph Murimi, Picha na Tryphone Odace

Alisema uwepo wa huduma za kibingwa za macho katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga utapunguza ulazima wa wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu, hali itakayosaidia kupunguza gharama na muda wanaotumia kutafuta huduma hizo.

“Uwepo wa huduma hizi utakuwa chachu ya kuboresha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi, kwani utawasaidia kupata huduma karibu na maeneo yao na kupunguza safari ndefu za kutafuta matibabu,” amesema Murimi.

Naye Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola, aliahidi kuwa Kanisa litaendelea kusimamia utunzaji wa mradi huo ili kuhakikisha jengo na vifaa vilivyowekwa vinatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Alisema dhamira ni kuhakikisha huduma za afya ya macho zinaendelea kutolewa kwa ubora unaostahili na kuwanufaisha wananchi wanaozihitaji.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Meneja Mkazi wa Programu wa Shirika la Tanzaneye, Ryner Linuma, alisema ujenzi wa jengo hilo pamoja na ununuzi wa vifaa vya kutolea huduma umegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.

Linuma amesema Tanzaneye linaendelea kuwekeza katika kuongeza idadi ya wataalamu wa afya ya macho pamoja na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma hizo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupanua wigo wa upatikanaji wa matibabu ya macho nchini.

Meneja Mkazi wa Programu wa Shirika la Tanzaneye, Ryner Linuma, Picha na Tryphone Odace

Alieleza kuwa uwekezaji huo unalenga kuimarisha uwezo wa vituo vya kutolea huduma za afya ya macho ili wananchi waweze kupata uchunguzi na matibabu yanayohitajika kwa urahisi zaidi.

Uzinduzi wa jengo hilo na huduma za kibingwa za magonjwa ya macho katika Hospitali ya Rufaa ya Kabanga unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine.

Huduma hizo zinatarajiwa kupunguza gharama za usafiri, muda wa kusafiri kutafuta matibabu na changamoto zinazowakabili wananchi wanaohitaji huduma za kibingwa za afya ya macho.

Muonekano wa jego lililozinduliwa, Picha na Tryphone Odace

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha miundombinu ya afya na kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi, hususan wale wanaokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa matibabu maalumu.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.