Skip to main content

ANGELINA PETER: MJASIRIAMALI ALIYEGEUZA HAPANA KUWA NDIYO, 'WALINIAMBIA NI NGUMU'

Na Ibrahim Rojala,Geita

ANGELINA PETER: MJASIRIAMALI ALIYEGEUZA HAPANA KUWA NDIYO, 'WALINIAMBIA NI NGUMU'


Na Ibrahim Rojala,Geita

“Waliniambia biashara ya udongo ni ngumu, kwamba sitaweza. Wengine walinishauri niendelee na biashara nilizokuwa nikifanya zamani. Lakini nilisema nijaribu. Hata nilipowahi kupata hasara ya shilingi laki tano baada ya mzigo wangu kulowa kwa mvua, sikukata tamaa.”

Haya ni maneno ya Anjelina Peter (49), mjane na mama wa watoto sita, mkazi wa Kitongoji cha Msufini katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, mkoani Geita.

Maneno yake yanaeleza kwa ufupi safari ambayo haikuwa ya kawaida, safari iliyopitia maumivu ya kumpoteza mwenza, mzigo wa kulea watoto, kukatishwa tamaa, kupata hasara na hatimaye kugeuza mtaji mdogo kuwa chanzo cha matumaini na mafanikio ya familia.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya wajane 1,396,262, sawa na asilimia 4.4 ya wanawake wote nchini.

Nyuma ya takwimu hizo kuna simulizi nyingi za wanawake wanaopambana na maisha baada ya kupoteza wenza wao, kwa Anjelina, ujane haukuja peke yake; ulikuja pamoja na jukumu la kulea watoto sita.

Watoto wake watano walimpoteza baba yao wakiwa bado wadogo, wakati Anjelina akiwa mjamzito wa mtoto wa sita.

Kuanzia hapo, maisha yakabadilika,kwani alibaki akiwa hana chaguo la kukaa na kusubiri msaada, Anjelina alilazimika kufanya shughuli mbalimbali kama vile kuuza viazi mvringo kwa bei ya jumla,alivyokuwa akivitoa Namanga na kuuza kwa bei ya jumla mkoani Mwanza,kuuza samaki,kutembeza mbogambobga na nyanya ili kuhakikisha watoto wake wanapata mahitaji muhimu na kukua katika mazingira bora.

Akiwa katika harakati hizo za kutafuta maisha siku moja alinusurika kufa maji baada ya mtumbwi aliutumia kufuata samaki visiwani kutaka kuzama,baada ya mihangaiko mingi ndipo aligundua jambo moja muhimu, fursa wakati mwingine haiji ikiwa imefungwa kwenye bahasha ya fedha inaweza kuja kupitia mtu anayekupa wazo.

Na kama ambavyo wahenga walivyowahi kusema mtembea bure si sawa na mkaa bure,Anjelina alipoendelea kutangamana na watu na kusikiliza mawazo mbalimbali, ndipo alipopata taarifa kuhusu biashara ya udongo unaojulikana kama pemba.

“Kulikuwa na rafiki yangu alikuwa akifanya biashara ya udongo,akaniambia biashara hii inasaidia na imemtoa kimaisha ha hivyo akanishauri kuijaribu,ndipo nikaanza rasmi biashara hii”anasema Anjelina

Wazo hilo likawa mwanzo wa sura mpya katika maisha yake,lakini mwanzo haukuwa mwepesi kwani kabla hajaanza, baadhi ya watu walimkatisha tamaa. Wengine walimwambia biashara ya udongo ni ngumu na hataweza. Wengine walimshauri aendelee na biashara zake za awali,hata hivyo, Anjelina akaamua kujaribu.

“Watu walinicheka sana,wengine walisema pemba ya shilingi 100 nitauza ngapi mpaka nije kufanikiwa,lakini sikukata tama,kuna siku  moja mvua ilinyesha,udongo niliokuwa nimeanika uliokuwa na thamani ya shilingi 500,000 ukaloana wote,nililia japo sikutoa lakini nililia moyoni nililia moyoni”anaeleza Anjela

Alikutana na changamoto hivyo iliyomfundisha kuwa hasara si lazima iwe mwisho wa safari,kwa mtu anayejenga biashara kutoka kwenye mtaji mdogo, hasara hiyo ingeweza kuwa sababu ya kufunga ukurasa na kurudi nyuma.

Lakini Anjelina hakukata tama,aliendelea na polepole, biashara ikaanza kupata wateja, soko likaanza kufunguka na hapo ndipo akaona kuwa katika biashara, ubunifu ni sehemu ya mafanikio.

Wakati nikifanya nae mahojiano nilimkuta Anjelina akifunga oda za wateja walioagiza udongo kutoka katika maeneo mbalimbali ya nje ya Mji mdogo wa Katoro kama vile Lwamgasa na Mgusu na hali hiyo imechochewa na ubunifu ambao Anjelina pamoja na timu yake ya uzalishaji wakaamua kubadili namna ya kuiwasilisha bidhaa hiyo.

Pemba ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikihusishwa zaidi na matumizi ya wajawazito, sasa wakaanza kuitengeneza kwa ubunifu mwingine na kuipata pemba yenye ladha ya limao.

Huo ukawa mwanzo mwingine wa safari yake,kutoka kwenye mtaji wa shilingi 50,000, biashara hiyo imeanza kubadilisha maisha ya Anjelina na familia yake.

Leo, anasimulia mafanikio ambayo hapo awali huenda yalionekana kama ndoto: ameweza kujenga nyumba nzuri ya kisasa, kusomesha watoto wake na kuboresha maisha ya familia.

Lakini mafanikio yake hayakuishia kwake,kupitia biashara hiyo, amekuwa pia akiwapa wanawake wengine nafasi ya kujishughulisha na kujipatia kipato, akiamini kwamba mwanamke akipewa nafasi na kuamua kupambana, anaweza kubadilisha maisha yake na ya familia yake.

Kutoka kwenye maumivu ya ujane, kupitia maneno ya waliomkatisha tamaa, hasara ya shilingi laki tano na mtaji wa shilingi 50,000, Anjelina sasa ana simulizi tofauti, ni simulizi inayosema kwamba maisha yanaweza kukupiga, lakini si lazima yakumalize.

 Na kupitia kipaza sauti cha Jambo Media, Anjelina anawafikishia ujumbe wajane wenzake na wanawake wanaoishi kwa kutegemea wanaume pekee kwa kuwasihi  wasikae wakisubiri msaada, bali wajitafutie shughuli za kuwaingizia kipato, wajifunze, wabuni na kutumia fursa zinazowazunguka.

Kwa sababu kwake, pemba haikuwa tu biashara ya udongo, ilikuwa daraja lililomvusha kutoka kwenye kipindi kigumu cha maisha kwenda kwenye matumaini mapya huku akipata uungwaji mkono kutoka kwa watoto wake.

Na huo ndio ushahidi kwamba wakati mwingine, mtaji wa mafanikio si fedha nyingi  bali ni ujasiri wa kuanza.

Join the conversation

What do you think about this story?

Share a useful perspective and keep the discussion respectful.

Keep reading

View all news
ON AIR
Jambo Assistant Tayari kukusaidia
JAMBO FM INTELLIGENCE

Kikomo cha maswali 6 kimefikiwa.Jaribu tena baada ya .
Utafiti utafunguka kwenye ukurasa kamili

Majibu ya AI yanaweza kuwa na makosa.