Na Eunice Kanumba – Morogoro.
Serikali imedhamiria kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kwamba kwasasa ajenda hiyo imepewa kipaumbele lengo likiwa ni asilimia 80 ya watanzania kwa kaya watumie nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 kutoka asilimia 28.6 ya sasa huku Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa mawasiliano utakaowezesha wananchi wengi zaidi kupata elimu na kuhamasika kutumia nishati hiyo.
Hayo yameelezwa leo tarehe 15 july 2026 na naibu waziri wa nishati Salome Makamba wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa ajili ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari, Maafisa Habari na Maafisa Mawasiliano wa Serikali kuhusu uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia katika ukumbi wa Karena uliopo katika manispaa ya Morogoro.

Warsha hiyo imeandaliwa na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji (UNCDF), kupitia Mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya.
Makamba amewataka waandishi wote wa habari kuendelea na kampeni kwa kuandika habari za nishati safi ya kupikia kwa usahihi ili jamii hasa waishio maeneo ya vijijini kufahamu faida za nishati safi ya kupikia na kubadili mtazamo juu ya nishati za kale kama kuni na mkaa ambazo zinapelekea ukataji wa miti na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka wizara ya nishati Nolasco Mlay amesisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa sahihi kuhusu nishati safi ili kujenga uelewa kwa wananchi, huku akianisha kuwa waandishi wa habari wana nafasi muhimu katika kuondoa upotoshaji wa taarifa na kuhamasisha jamii kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya afya, mazingira na maendeleo ya uchumi.
Naye Meneja wa Cook Fund kutoka UNCDF, Emmanuel Muro, amesema mradi huo unalenga kuchochea ukuaji wa soko la nishati safi na kuongeza mwitikio wa wananchi katika matumizi ya teknolojia za kupikia kwa nishati safi.

Muro amewataka waandishi wa habari kuwa chachu ya mabadiliko kwa kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii, huku akibainisha kuwa bado kuna changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi zinazohitaji kuendelea kutatuliwa kupitia elimu na ushirikiano wa wadau.
Nao baadhi ya waandishi wa habari na mafisa habari na mawasiliano kutoka katika taasisi za umma walioudhuria warsha hiyo wameipongeza wizara ya nishati kwa kushirikiana na mfuko wa maendeleo ya mitaji (UNCDF) kwa kuandaa warsha hiyo ambayo imewajengea uwezo na kwamba wanakwenda kuwa mabalozi wazuri katika jamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Wananchi wanahimizwa kutumia nishati safi kama gesi ya kupikia (LPG), umeme, biogas na majiko banifu, ambayo husaidia kupunguza gharama za muda mrefu na kuhifadhi misitu. Wataalamu wanaeleza kuwa matumizi ya nishati safi pia huokoa muda unaotumika kutafuta kuni na kuongeza usalama ndani ya kaya.
Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za nishati safi ya kupikia, huku wadau mbalimbali wakishirikiana kuendelea kutoa elimu na kuongeza upatikanaji wa teknolojia hizo nchini.

Discussion
Reader comments
0 contributions