Na Ibrahim Rojala, Bukombe - Geita.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, ameeleza kuwa hakuna madhara kwa binadamu, ikiwemo vifo yaliyojitokeza kufuatia kuporomoka kwa maduara manne katika Mgodi wa dhahabu wa Msasa uliopo wilayani Bukombe tukio lililotokea Machi 29, 2026
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio wakati zoezi la utafutaji likiendelea, SACP Safia Jongo ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo hilo ili kuzuia uhalifu na kulinda usalama wa raia pamoja na mali zao akitoa wito wa watu kujiepusha na usambazaji wa taarifa potofu kwa lengo la kuzua taharuki jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

‘Naomba nichukue fursa hii nijulishe umma wa watanzania kwamba mgodi wa Msasa ni salama na kutokana na kutitia kwa mashimo haya hakuna madhara yoyote kwa binadamu,hayapo kwasababu tumeshafikia zaidi ya asilimia 97 lakini hakuna dalili yoyote ya binadamu kuwepo’amesema
Aidha amebainisha kwamba kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Geita kwa kutambua kuwa matukio kama hayo hutokea nyakati za mvua,iliamua kuendesha mafunzo katika migodi yote ya wachimbaji wadogo mkoani humo,elimu ambayo imechangia kupunguza madhara pindi matukio ya aina hiyo yanapojitokeza.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, ASF Keneth Mwakasitu amesema zoezi la utafutaji linaendelea kufanyika kwa weledi mkubwa kwa kushirikiana na wananchi, ambapo tayari baadhi ya mali zilizokuwa zikitumika katika shughuli za uchimbaji zimepatikana.
‘Wengi wanachanganya utafutaji na uokoaji,zoezi lililopo sasa hivi ni la utafutaji, kama kutatokea kuna mabaki au viashiria vya watu wowote walionasa tutasema tunaanza uokoaji,lakini zoezi lililopo sasa hivi ni la utafutaji na muda si mrefu tutakamilisha zoezi hili,’ amesema ASF Mwakasitu.

Aidha amewataka wachimbaji kuendelea kuchakua tahadhari wakati wa utekelezaji wa majukumu yao hususani katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.
Naye Chifu Mkuu wa Mgodi wa Msasa, James Nkamba, ameeleza kuwa zoezi hilo limeendelea vizuri, huku juhudi zikielekezwa katika kuhakikisha mali zote zilizofukiwa zinapatikana na kuhakikisha usimamizi katika eneo hilo, ili kulinda maisha ya watu na mali zao na kuendesha shughuli za uchimbaji katika hali ya usalama.

Discussion
Reader comments
0 contributions