Kampuni ya Joby Aviation imefanya jaribio la kuendesha ndege kwa kutumia mfumo wa akili mnemba unaowezesha safari kufanyika bila uhitaji wa rubani katika uendeshaji wa ndege moja kwa moja. Ndege hiyo aina ya Cessna 208 Caravan ilisafiri kutoka California hadi North Carolina nchini Marekani, umbali wa takribani kilomita 5,148, huku mfumo huo ukisimamia hatua mbalimbali za safari kama vile kupaa, kufuata njia, kubadilisha mwelekeo na kutua. Rubani alikuwepo ndani ya ndege kwa ajili ya usalama na kutimiza matakwa ya kanuni, lakini kwa mujibu wa kampuni hiyo hakuhitajika kuingilia udhibiti wa ndege wakati wa safari.

Kinacholifanya jaribio hili kuwa la kipekee si umbali ambao ndege hiyo ilisafiri, bali ni aina ya majukumu ambayo akili mnemba iliweza kuyatekeleza. Kwa kawaida, safari ya ndege huhitaji rubani kufuatilia mazingira, taarifa za ndege, hali ya hewa na mabadiliko ya njia, kisha kufanya maamuzi kwa wakati unaofaa. Katika jaribio hili, mfumo uliweza kuchanganua taarifa hizo na kutekeleza hatua mbalimbali za safari bila kuhitaji rubani kutoa kila agizo. Teknolojia hiyo imefanyiwa majaribio katika safari zaidi ya 400 na imekusanya zaidi ya saa 800 za safari za kujiendesha katika mazingira mbalimbali ya anga.
Hatua hii inaonyesha mabadiliko makubwa katika namna akili mnemba inavyotumika. Kwa muda mrefu akili mnemba imekuwa ikitumika zaidi kuchanganua taarifa, kutafsiri lugha, kutengeneza maudhui au kumsaidia binadamu kufanya maamuzi. Lakini kwa sasa teknolojia hiyo inaanza kuunganishwa na mashine zinazoweza kutambua mazingira, kuchanganua taarifa na kuchukua hatua zenyewe. Hii ina maana kwamba akili mnemba inaanza kutoka kwenye ulimwengu wa programu za kompyuta na kuingia katika ulimwengu halisi, ambapo maamuzi yake yanaweza kuathiri moja kwa moja usafiri, uzalishaji na usalama wa binadamu.
Iwapo teknolojia hii itaendelea kukomaa, matumizi yake yanaweza kuanza katika maeneo ambayo hayahitaji uwepo wa abiria, kama vile ndege za mizigo, usafirishaji wa dawa, shughuli za uokoaji na safari katika maeneo hatarishi. Badala ya kuondoa rubani mara moja, huenda hatua ya kwanza ikawa ni kumpunguzia baadhi ya majukumu, huku akili mnemba ikisimamia kazi zinazoweza kufanywa kwa usahihi na kwa mwendelezo. Baadaye, ikiwa itakidhi viwango vya usalama na kanuni baadhi ya ndege zinaweza kuendeshwa kwa kiwango kikubwa zaidi bila rubani ndani.
Hata hivyo, jaribio hili halimaanishi kwamba ndege za abiria zitaanza kusafiri bila marubani hivi karibuni. Usafiri wa anga unahitaji kiwango cha juu sana cha usalama, hivyo teknolojia kama hii italazimika kupitia majaribio mengi, tathmini za kina na uthibitishaji kutoka kwa mamlaka husika. Mfumo unapaswa pia kuthibitisha kwamba unaweza kukabiliana na hali zisizotarajiwa, hitilafu za vifaa, mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira mengine ambayo hayakupangwa wakati wa safari.

Swali kubwa ambalo halina majibu hadi hivi sasa ni je ikiwa ndege inayoendeshwa na akili mnemba itafanya uamuzi usio sahihi na kusababisha ajali, nani atawajibika? Je, ni kampuni iliyotengeneza mfumo huo, kampuni inayomiliki ndege, msimamizi wa safari au mtu aliyesanidi mfumo? Maswali haya yanaonyesha kwamba changamoto ya ndege zinazojiendesha si ya kiteknolojia pekee, bali pia ni ya kisheria na kiusalama. Ni lazima kuwe na utaratibu unaoeleweka wa kugawa majukumu na kuhakikisha kwamba binadamu anaweza kuingilia kati pale mfumo unaposhindwa kufanya uamuzi sahihi.
Jaribio la Joby Aviation linaweza kuwa sehemu ya mwanzo wa mabadiliko mapana zaidi katika matumizi ya akili mnemba. Teknolojia hiyo inaweza baadaye kuboreshwa katika magari yanayojiendesha, roboti za viwandani, maghala, kilimo na huduma za dharura, ambapo mashine zitahitaji kutambua mazingira, kufanya maamuzi na kuchukua hatua bila kusubiri binadamu kutoa kila agizo. Kinachoendelea kwa sasa kinaonyesha kwamba mjadala kuhusu akili mnemba sasa hauhusu tu uwezo wa kompyuta kufikiri au kuchakata taarifa, bali unaelekea kwenye swali kubwa zaidi: tuko tayari kwa kiwango gani kuzipa mashine uwezo wa kufanya maamuzi katika ulimwengu halisi?
Discussion
Reader comments
0 contributions