Historia mpya imeandikwa kwenye sekta ya elimu nchini, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuamua kuzifuta kanuni zilizokuwa zikiruhusu wanafunzi kuchapwa viboko shuleni.
Katika hukumu iliyotolewa Novemba 3, 2026 kupitia Usajili wake wa Dodoma, Mahakama hiyo imesema kanuni hizo ni kinyume na Katiba, kwa sababu zinamvunjia mwanafunzi haki yake ya kuheshimiwa kama binadamu na kumweka kwenye adhabu za kikatili na za kudhalilisha.
Kanuni zilizofutwa.
Mahakama imezibatilisha Kanuni za 2, 3 na 6 za Kanuni za Elimu kuhusu Adhabu ya Viboko za mwaka 2002, ambazo zilitangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 294.

Uamuzi huo umetolewa na jopo la majaji watatu - Amir Mruma, Hassan na Irene Musokwa.
Kwa mujibu wa jopo hilo, kanuni hizo zinakwenda kinyume na Ibara ya 12(2) na 13(6)(e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi yafunguliwa.
Shauri hili lilifunguliwa mwaka 2025 na Samweli Maduhu Mangu, dhidi ya Waziri wa Elimu, akisaidiwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Chanzo cha kesi hiyo ni kifo cha kusikitisha cha Mhoja Maduhu, mwanafunzi wa Kidato cha Pili.

Mhoja alifariki dunia Februari 26, 2025, katika Shule ya Sekondari Mwasamba iliyopo wilayani Busega, mkoani Simiyu.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio, Mwalimu alimwadhibu kwa kuchapwa kwa sababu hakumaliza kazi ya kikundi ya somo la Jiografia. Katika tukio hilo, inadaiwa alipigwa sehemu mbalimbali za mwili, akiwemo kichwani, wakati akijaribu kujikinga.
Wanafunzi wengine ambao nao hawakumaliza kazi hiyo pia wanadaiwa kuadhibiwa siku ya tukio.

Discussion
Reader comments
0 contributions