Na Saulo Stephen - Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameagiza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kwa kushirikiana na Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kuhakikisha stendi zote bubu zinafungwa ndani ya wiki mbili, huku akisisitiza kuwa ni marufuku kwa mabasi kupakia au kushusha abiria na mizigo nje ya stendi na vituo rasmi vilivyoidhinishwa na Serikali.
Maagizo hayo yametolewa katika kikao cha usuluhishi wa mgogoro wa usafirishaji na matumizi ya stendi kilichowakutanisha viongozi wa serikali, LATRA, Halmashauri, mawakala wa mabasi, wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo na wadau wengine wa sekta ya usafirishaji Mkoa wa Singida.

Rc Dendego amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kujenga stendi za kisasa kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri, kuongeza mapato ya serikali na kuchochea shughuli za kiuchumi, hivyo hakuna sababu ya kuruhusu baadhi ya mabasi na mawakala kuendesha shughuli zao nje ya maeneo rasmi.
“Nawapa wiki mbili LATRA na Halmashauri mkafunge stendi zote bubu. Mabasi yote lazima yaingie stendi. Haiwezekani tuwe na stendi nzuri zilizojengwa kwa gharama kubwa halafu zisitumike wakati shughuli zinafanyika pembeni. Huu ni upotevu wa mapato na kuhujumu juhudi za Serikali,” alisema.

Aidha, ameagiza utolewaji wa elimu kwa wananchi, madereva, makondakta na mawakala kwa siku saba kabla ya kuanza utekelezaji mkali wa sheria, akibainisha kuwa baada ya kipindi hicho hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote watakaokiuka utaratibu uliowekwa.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amesisitiza umuhimu wa kuboresha mazingira ya stendi kwa kuhakikisha huduma muhimu kama vyoo bora, maeneo ya chakula, usafi wa mazingira, sehemu za kupumzikia abiria na miundombinu mingine inapatikana ili kuvutia wasafiri na kuongeza fursa za biashara kwa wananchi.

Sambamba na hayo, Dendego pia amewataka wadau wote kutatua changamoto zao kwa njia ya mazungumzo na ushirikishwaji badala ya maandamano, akieleza kuwa maendeleo hupatikana kupitia majadiliano yenye lengo la kupata suluhisho la kudumu.
Discussion
Reader comments
0 contributions