Na Eunice Kanumba –Shinyanga.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya ujenzi vinavyotumika katika ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), kufuatia operesheni maalum iliyofanyika ndani ya mwezi Machi 2026.
Akitoa taarifa juu ya kukamatwa kwa vifaa hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishina Msaidizi Mwandamizi (ACP) Janeth Magomi amesema, operesheni hizo zilianza Machi 1 - 31, 2026 zikiwa na lengo la kukabiliana na vitendo vya uhalifu katika kuhakikisha ulinzi wa raia na mali zao.
Amesema, katika operesheni hiyo, jumla ya watuhumiwa 35 walikamatwa katika Wilaya za Msalala na Shinyanga wakihusishwa na wizi wa vifaa hivyo.

Vifaa vilivyokamatwa ni pamoja na vipande 306 vya nondo, mabomba 32 makubwa ya milimita 12, stendi za makarasha 12 pamoja na mabomba ya mraba (square pipe) 65.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Tanzania kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kimeendesha operesheni dhidi ya madereva waliokiuka sheria, ambapo baadhi yao wamebainika kuendesha vyombo vya moto bila leseni na wengine kuendeha vyombo vya moto kwa mwendo kasi uliopitiliza yaani kilomita 80 kwa saa.
Katika ukaguzi huo, jumla ya makosa 5,648 ya barabarani yalirekodiwa, yakihusisha magari 4,044 pamoja na pikipiki na bajaji 1,604, ambapo wahusika walitozwa faini kwa mujibu wa sheria.
Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi Tanzania kwa kutoa taarifa za uhalifu na kuzingatia usalama wao, kwani ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao pamoja na miradi ya maendeleolakini pia kudumisha amani katika jamii.
Discussion
Reader comments
0 contributions