Mamlaka ya usalama wa usafirishaji nchini Kenya imeomba ajali za barabarani kutangazwa kuwa "Janga la Kitaifa" kufuatia ajali mbaya ya Basi kugongana uso kwa uso iliyogharimu maisha ya watu 24 kwenye barabara kuu inayounganisha jiji la Nairobi na Mombasa.

Ajali hiyo ilitokea asubuhi ya Oktoba 25, 2026 wakati basi la abiria lilipogongana na lori (trela), na kuarifiwa kuwa abiria waliokuwa kwenye basi hilo walikuwa wakirejea jijini Mombasa wakitokea eneo la Magharibi mwa Kenya, ambako walikuwa wamehudhuria mazishi ya mchungaji wa kanisa lao.
Duru kutoka nchini zimeripoti kuwa mbali na vifo hivyo 24, watu wengine 24 wamejeruhiwa vibaya na kuwahishwa hospitalini kwaajili ya matibabu.
Mamlaka nchini Kenya zimeeleza kuwa ajali hiyo ilitokana na overtaking ya madereva bila umakini.

Manusura wa ajali hiyo Mchungaji Spencier Mdave, ambaye alikuwa mmoja wa abiria waliokuwemo ameelezea namna ajali hiyo ilivyowakumba.
"Sisi tulioshuhudia mkasa huu tunasema kwamba trela lilijaribu kulipita basi letu, lakini likakutana na magari yaliyokuwa yakija mbele. Dereva wa trela alipojaribu kusitisha zoezi hilo la kulipita basi, ndipo alipopoteza udhibiti wa gari.
"Watu waliopata majeraha mabaya zaidi ni wale waliokuwa wameketi nyuma ya basi. Sisi tuliokuwa mbele tuko afadhali na hata wengi wetu tumesharuhusiwa. Kama mimi, nimepata tu mchubuko mdogo na nimekuwa hapa tangu ajali itokee lakini sisikii maumivu yoyote mwilini." Spencier Mdave
Ajali hii hiyo imetokea wiki tatu tu baada ya ajali nyingine iliyogharimu maisha ya watu 17 kutokea katika barabara hiyo hiyo kuu inayounganisha mji mkuu wa Nairobi na mji wa bandari wa Mombasa.
Maafisa wa usalama barabarani nchini Kenya sasa wanashinikiza ajali za barabarani kutangazwa rasmi kuwa "Janga la Kitaifa", wakibainisha kuwa takriban ajali 20,000 zinazotokea nchini humo hugharimu maisha ya zaidi ya watu 5,000 kila mwaka.

Kufuatia hayo Rais wa Kenya, William Samwel Ruto, ametuma salam za rambirambi kwa familia zilizowapoteza wapendwa wao na kuagiza ukaguzi wa kina mara moja, ufanyike kwa magari yote ya abiria (PSV) ili kuhakikisha yanazingatia sheria na kuondoa ajali barabarani, na hkuku akiwasihi madereva wote kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani:
"Ninawasihi madereva kuwa waangalifu zaidi na kuzingatia sheria za barabarani ili kulinda maisha ya wananchi," amesema Wilium Samwel Ruto.
Discussion
Reader comments
0 contributions