Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameitisha mkutano mwingine wa dharura wa baraza lake la ulinzi na usalama leo kwa ajili ya kujadili ghasia zinazoendelea katika kisiwa cha New Caledonia ambacho ni himaya yake.
Huu ni mkutano wa tatu kuitishwa na Macron chini ya wiki moja, mikutano ya awali ilitoka na maamuzi ya kutangaza hali ya hatari kutuma Wanajeshi ili kusaidia vikosi vya serikali ya kisiwa hicho kurejesha utulivu,hapo jana, wanajeshi wa Ufaransa walikuwa na kazi ya kuondoa vizuizi katika barabara kuu inayoelekea uwanja wa ndege. Mnamo siku ya Ijumaa waziri mkuu wa Ufaransa Gabriel Attal alikutana na viongozi wa vyama vya siasa bungeni kujadili mgogoro huo na haswa suala la kurefusha hali ya hatari baada ya siku 12 za awali.
Kisiwa cha New Caledonia kinapatikana, Kusini mwa bahari ya Pasifiki, Mashariki mwa Australia na kiko chini ya himaya ya Ufaransa,bunge la Ufaransa mjini Paris limekuwa likijadili muswada wa kufanya mageuzi ya katiba ya kisiwa hicho ili kuwapa fursa raia wake wasiokuwa wenyeji wa kisiwa hicho kuwa na haki ya kupiga kura.
Lakini baadhi ya viongozi wa New Caledonia wanahofia muswaada huo utayavunja nguvu maamuzi ya wakaazi asilia wa kisiwa hicho kupitia michakato ya uchaguzi Na mageuzi hayo ya sheria ya uchaguzi ndiyo mvutano wa hivi karibuni kabisa katika mapambano ya miongo kadhaa ya watu wa New Caledonia kuhusu dhima ya Ufaransa ndani ya kisiwa hicho.
Maandamano yaliyoshuhudiwayamezichochea mamlaka kufunga uwanja wake wa ndege wa kimataifa na kutangaza hatua ya kuzuia watu kutembea katika mji mkuu Noumea pamoja na kupelekwa kwa maafisa wa polisi kuweka usalama huku maduka na magari yakiteketezwa.