Na Faustine Kasala – Kigoma.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Levocutus Chipando maarufu kama Baba Levo, amesema wananchi wa jimbo la Kigoma mjini wanatamani kumuona akigonga meza za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kampeni za Chama hicho uliofanyika katika uwanja wa MWANGA COMMUNITY CENTER Manispaa ya Kigoma ujiji, Septemba 9, 2025 Baba Levo amesema, atakaye jaribu kuizuia ndoto hiyo atadhalilika asubuhi siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025.

“Najua mnafahamu nilivyo wapambania nikiwa katika nafasi ya udiwani,mnafahamu pia upendo nilionao katika mji huu, ndiyo maana CCM imenirudisha kuwa mgombea wa Jimbo la Kigoma mjini, na ninafamu kuwa mnayo ndoto ya kumuona Baba Levo BABA LA BABA likingonga meza za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Sasa niwaambie atakaye jaribu kuizuia ndoto hii atadhalilika asubuhi mapema siku ya Uchaguzi,” amesema Baba Levo
Aidha, Baba Levo ameeleza vipaumbele katika uongozi wake endapo ataaminiwa na wananchi wa Jimbo hilo kuwa ni pamoja na kuhakikisha anafuta Barabara zote za vumbi katika mji wa Kigoma,kuhakikisha vijana wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu hususani Maafisa usafirishaji na Machinga pamoja na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatekelezwa na inayo tarajiwa kutekelezwa na Serikali katika jimbo hilo.
Naye Naibu Waziri wa TAMISEMI, Zainabu Katimba akizungumza na Wananchi waliojitokeza katika ufunguzi wa Kampeni za chama hicho amewataka wananchi kujitokeza kupiga kura kwa wingi kwa wagombea wote wa chama cha Mapinduzi CCM kutokana na Miradi mbalimbali ya maendeleo iliyo tekelezwa na Serikali katika mkoa wa Kigoma
“Ndugu zangu nataka niwaambie hatuna sababu ya kuacha kumpigia kura nyingi na za kutosha Mama yetu Samia Suluhu na wagombea wengine wote kutoka CCM, Shughuli za Maendeleo zilizofanyika hapa Kigoma zinajieleza Masoko yamejengwa na yanaendelea kujengwa, Meli zinakarabatiwa uwanja wa ndege huo,Mambo ambayo yanazidi kuongeza fursa za Kiuchumi katika mkoa wetu wa Kigoma,” alusrma Zainabu.
Kwa upande wake Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Kigoma, Cristopha Parangyo akiinadi Sera ya chama hicho kwa mwaka huu wa uchanguzi 2025 amesema pamoja na mambo mengine Sera hiyo imelenga kuinua uchumi wa kila Mtanzania, kuwarasmisha waendesha Bodaboda katika sekta ya usafirishaji,Bima ya Afya kwa kila mtu,ujenzi wa Miundobinu, Masoko na mengineyo.


