Na Saada Almasi -Simiyu
Mamlaka ya bodi ya Pamba Wilayani Bariadi mkoani Simiyu imepokea ndege nyuki tano zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutumika kunyunyiza dawa za kuua wadudu katika mashamba ya wakulima zaidi ya elfu 50 wilayani humo ili kuwarahisishia upatikanaji wa mavuno yenye tija.
Mkaguzi wa Pamba wilayani Bariadi Ndinda Anthony amesema kuwa hadi sasa wilaya hiyo ina ekari zaidi ya elfu 74 zinazolimwa zao hilo ambazo zilikuwa zikihudumiwa na ndege nyuki moja iliyokuwepo katika wilaya hiyo lakini kwa sasa ndege hizo zinakwenda kuhudumia wakulima wote bila kujali ekari alizonazo na bila gharama yoyote.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/NDEGE-1024x768.jpeg)
“Tuna hakika hizi ekari zaidi ya elfu 74 ambazo zimelimwa na kupandwa vizuri na wakulima wetu zilizokuwa zikihudumiwa na ndege nyuki moja sasa zinaenda kunufaika kwa kuhudumiw na hizi zingine tano na kwa kuwa hazina gharama yoyote ya kunyunyiza zitakwenda kuhudumia kila mkulima bila kujali ana ekari ngapi atafikiwa” – Ndinda Anthony.
Sambamba na hilo Ndinda amewataka wakulima wote kuweka mazingira rahisi ya kufanikisha unyunyizaji huo kwa kuhakikisha mashamba yao hayana miti mirefu ambayo inakuwa kikwazo kwa ndege nyuki kupaa na kuhudumia eneo hilo.
“Nawaomba wakulima wote wahakikishe katika mashamba yao hakuna vizuizi kama vile miti mirefu lakini pia eneo liweze kufikika kunapokuwa na miti mirefu ndege nyuki haiwezi kuruka na kunyunyiza hivyo wahakikishe kunakuwa na mazingira rahisi ya kazi” – Ndinda.
Ndege nyuki hizo ambazo kwa sasa zimekuwa sita kwa wilaya ya Bariadi pekee si tu zinakwenda kupambana na vijidudu lakini pia zinakwenda kuondoa changamoto ya maradhi ya kifua na mgongo hususan kwa wakulima wenye ekari nyingi kutokana na kutumia pampu za mkono kupulizia mazao hali ambayo wakati mwingine walilazimika kutomaliza kupulizia eneo lote hivyo kupata mazao kidogo kama mmoja wa kwakulima hao Danford Segela.
“Mkulima anaenda kunufaika hata kama alime ekari ngapi atakuwa na uhakika wa mavuno mengi yenye tija tulikuwa tunakatishwa tamaa na kumwagilia kwa kubeba pampu mgongoni na baada ya muda mtu unapata maumivu ya kifua,mgongo na hata kuchoka unaamua tu kuacha kupulizia” – Danford.
![](https://jambofm.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/NDEGE-NYUKI-1024x683.jpeg)
Kwa upande wake Ndekwa Mageme ni mkulima na mnufaika wa huduma hiyo ambaye licha ya kuishukuru seikali kwa huduma hiyo pia ameiomba kuongezewa kwa idadi ya ndege nyuki hizo ili zisambazwe katika maeneo yote ya mashamba na kuwanufaisha wakulima wengi zaidi na hatimaye kuwa na kilimo chenye tija
“Tunaishukuru sana serikali tunaahidi kuhudumia mashamba yetu kwa ndege nyuki hizi lakini pia tunaomba ziongezwe zisambazwe sehemu nyingi ili wakulima wengi zaidi wafikiwe na huduma hii”
Kutokana na uwekezaji katika zao hilo wilaya ya Bariadi yenye halmashauri mbili yaani bBariadi mji na Bariadi vijijini inatarajia kupata zaidi ya kilo milioni 30 katika msimu wa 2024/2025 ambazo hazijawahi kupatikana hapo nyuma.