Mkazi wa Kijiji cha Mwakubilinga, Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, Ndakama Pauline Kisabo (35), amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Kwimba baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka binti yake wa kumzaa (10).
Hukumu hiyo imesomwa hii leo Mei 29, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ndeko Ndeko, katika kesi ya jinai namba 4924/2025, baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kiparo, tukio hilo lilitokea tarehe 9 Februari 2025 katika Kijiji cha Mwakubilinga, wakati bibi wa mtoto huyo alipowamuacha mtoto huyo kwa baba yake ambaye alishatengana na mama wa mtoto huyo ndipo mshatakiwa alimvuta mhanga na kumbaka kisha kumpatia elfu moja ili asilie.

Mshtakiwa alifikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 26 Februari 2025 na kusomewa shtaka la kuzini na maharimu, kinyume na Kifungu cha 158(1)(a) cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya 2022), ambapo alikana kutenda kosa hilo.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita, akiwemo mhanga na mama wa mshtakiwa ambaye alithibitisha Mahakamani kuwa mwanawe alitenda kosa hilo kwa mjukuu wake.
Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetetea, alilia na kudai kuwa mama yake mzazi amemuangamiza kwa kutoa ushahidi dhidi yake, akisisitiza kuwa hakutenda kosa hilo na kuiomba mahakama imsamehe.
Hata hivyo, upande wa mashtaka uliomba Mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine, ukieleza kuwa kitendo hicho si cha utu na kimeharibu maisha ya mtoto mdogo.
Akitoa hukumu, Hakimu Ndeko alisema kuwa kutokana na uzito wa kosa na athari zake kwa mtoto, Mahakama imemuadhibu kwa kifungo cha miaka 30 jela ili liwe fundisho kwa jamii nzima.