Nchimbi: Marekani ni rafiki zetu

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel John Nchimbi amesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora na hivyo haipaswi kutiliwa shaka hata kidogo.

Katibu Mkuu wa CCM ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Balozi Nchimbi amesema katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.

Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa CCM chini ya Rais Samia, kitahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo kwa kuunga mkono uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa maslahi ya nchi na taifa kwani umoja huo ni zaidi ya vyama vya siasa.

Katika mazungumzo yao, wamekubaliana nchi zote mbili kuangalia maeneo yanayoweza kuboreshwa kwa manufaa ya pande zote mbili hasa katika nyanja za biashara, uchumi na uwekezaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *