MZEE WASIRA ASEMA ILANI YA CCM INALENGA KUJENGA UCHUMI KUINUA HALI YA MAISHA.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa ilani yake ya uchaguzi inalenga kujenga uchumi jumuishi unaogusa na kuinua hali ya maisha ya kila Mtanzania kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi.

Kauli hiyo imetolewa Septemba 6, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara,Steven Wasira, alipokuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika jimbo la Musoma Mjini mkoani Mara.

“Ilani yetu inasema tunataka kujenga uchumi jumuishi unaolenga maendeleo ya mtu mmoja mmoja. Tuna wakulima katika mkoa wa Mara wanaopambana na changamoto za kilimo, hivyo tunahitaji kuboresha maisha yao kupitia sekta mbalimbali na kuwainua wananchi,”Amesema Wasira.

Aidha, Wasira ametumia nafasi hiyo kunadi ilani ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2025-2030 na kuwaombea kura mgombea urais Dkt.Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi, pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho kote nchini.

“Haya ndio mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunaposema tumpe kura, siyo zawadi bali ni kumshukuru kwa kazi kubwa aliyoifanya. Wapo wanaosema tunamsifu sana, lakini je, walitaka tumshukuru mtu ambaye hata darasa moja hajajenga?”amehoji Wasira.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji,amemshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha shilingi bilioni 19 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati katika Manispaa ya Musoma.Amesema fedha hizo zitasaidia kuleta maendeleo makubwa endapo wananchi watamchagua na kumpa nafasi ya kuzisimamia ipasavyo.

Aidha viongozi wa CCM wilaya ya Musoma Mjini wamewaomba wananchi kuendelea kuiamini CCM kwa kumpigia kura Dkt. Samia Suluhu Hassan,wagombea ubunge na madiwani wote wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao,wakisisitiza kuwa CCM ndiyo chachu ya maendeleo ya kweli kwa taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *