MWIZI AUAWA NA WENYE HASIRA KALI, KAMANDA JONGO AONYA UCHUKUAJI SHERIA MKONONI

Na. Frank Aman – Geita.

Mtu mmoja anayekadiliwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 32 ameuawa na Wananchi wenye hasira kali, wakimtuhumu kuhusika katika tukio la Wizi wa Mifugo lililofanyika Februari 8, 2025 majira ya Saa 11 alfajiri katika Kijiji cha Iponyamakalai kilichopo Kata ya Nyakamwaka Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Akizungumza katika Mahojiano maalumu na Jambo FM kuhusiana na Hali ya Usalama Mkoani humo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema tukio hilo lilitokea baada ya kundi la Wananchi kuwakuta Wezi hao wakiwa wamechinja Ng’ombe pembezoni mwa Mto na kuanza kupakia Nyama kwa ajili ya kwenda kuiuza.

Amesema, katika Wizi huo uliohusisha watu Wanne, Mmoja wao aliuawa papo hapo na Watatu kati yao walikimbia kusikojulikana ambapo Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta huku akiwataka Wananchi kutokujichukulia Sheria Mkononi na kuwataka kushirikiana na Jeshi hilo katika kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria.

Kuhusu hali ya Usalama Mkoani humo, Kamanda Jongo amesema Mkoa upo shwari na hakuna matukio makubwa ya kihalifu yaliyoripotiwa kutokea na kwamba wanaendelea kushrikiana na Vyombo vingine vya Usalama katika kuwabaini waharifu na kutumia ushirikiano na Wananchi kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *