Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunzi wote wenye sifa za kuandikishwa darasa la kwanza na kujiunga kidato cha kwanza wanasajiliwa ndani ya muda uliopangwa.
“Mwisho wa zoezi la kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na uandikishaji wa darasa la kwanza ni Machi 31. Agizo langu kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ni kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi mwenye sifa anapata nafasi ya kujiunga na masomo.”
Ndejembi ametoa agizo hilo leo Machi 6 2024 wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya zoezi la kuripoti kwa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Kilolambwani iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.
“Niwatake pia watendaji wa ngazi za chini kuanzia mtendaji wa kijiji/mtaa, mtendaji wa kata na tarafa wote wanakua mstari wa mbele kuhakikisha wanashirikiana na walimu wakuu wa shule za msingi ambao wanafunzi wao wamefaulu ili kuwabaini ambao wazazi wao watazuia watoto wao kutojiunga na masomo,” amesema Ndejembi.