Na Saulo Stephen – Singida.
Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameongoza kwa vitendo katika kutekeleza haki yake ya msingi ya kidemokrasia kwa kuboresha taarifa zake za Mpiga Kura katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Misigiri, Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida.
Uboreshaji huu ni sehemu ya Awamu ya Pili ya zoezi la kitaifa la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la mpiga Kura na Uwekaji Wazi wa Daftari la Awali, linaloendelea kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei 2025, huku Vituo vyote vikiwa. Vinapokea wananchi kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni kila siku.

Dkt. Nchemba amesisitiza umuhimu wa kila Mwana singida na Mtanzania kutumia haki na wajibu huo wa kikatiba kwa kujitokeza kuboresha taarifa zao, kuhakiki usahihi wa taarifa, na kuhakikisha kuwa wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu ujao. Amesema: “Uchaguzi ni haki, ni wajibu, na ni chombo cha kulinda amani, maendeleo na usalama wa Taifa letu. Tujitokeze wote” amesisitiza Dkt. Chemba.

Sanjari na hayo amewasihi wananchi wote wanaohitaji kuboresha taarifa zao na wale wanaojiandikisha kwa mara ya kwanza au kuthibitisha majina yao katika daftari, wahakikishe wanajjtokeza kwa wakati kwenye vituo vyao.