MWENGE WA UHURU WAZINDUA DARAJA KIUNGO CHA VIJIJI VINNE MEATU

Na Saada Almasi – Meatu.

Kiongozi wa Kitaifa wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ussi ameweka jiwe la msingi katika mradi wa Daraja la Mwanyahina linalounganisha vijiji vinne vya Mwanyahina, Mwijidalala, Bushwahilini na Mwagwidila Wilayani Meatu Mkoani Simiyu lililokuwa halipitiki, hasa kipindi cha mvua.

Akizindua mradi huo, Ussi ameipongeza Mamlaka ya Barabara Vijijini (TARURA), kwa kutekeleza mradi huo kwa gharama ndogo ukilinganisha na kiasi cha fedha kilichopendekezwa.

“Kipekee nikupongeze meneja wa TARURA wilaya ya Meatu kwa utekelezaji mkubwa kwa gharama ndogo,hapa palitakiwa kujengwa kwa shilingi bilioni moja lakini ukasema hapana nitatekeleza kwa chini ya hiyo gharama na matokeo tunayaona,kwa kiwango hiki wananchi wanauhakika wa kutumia daraja kwa zaidi ya miaka kumi bila kuharibika hongera sana,” anesema Ussi.

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo Meneja TARURA wilaya ya Meatu Elieza Mayengo amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo umetekelezwa kwa zaidi shilingi milioni 396.5 na unatarajiwa kukamilika Agosti 26, 2025.

“Pamoja na changamoto ya mvua ambayo tulikutaka nayo katika mradi huu tunategemea kukamilisha na kuanza kutumika mnamo Agosti 26 ili adha ya mawasiliano waliyokuwa wanapitia wakazi wa vijiji hivi vinne iweze kuisha,” amesema Mayengo.

Jambo Fm imezungumza na Mwainga Maduhu, mkazi wa Mwanyahina na Stella Boniface mkazi wa Mwajidalala na kusema kuwa haikuwa mara moja kushindwa kufika sokoni kufuata mahitaji muhimu humu Mwainga akieleza matukio ya vifo vya watoto kutokana na kujaa mto huo kipindi cha masika.

“Kutoka hapa kwenda sokoni haikuwa rahisi inabidi uwahi kabla ya mvua kunyesha tofauti na hapo mtakaa nyumbani bila chochote,” amesema Stella.

“Tulilazimika kuondoka asubuhi kusindikiza watoto shule maana anaweza kubebwa na maji ya mto,wakati mwingine wakienda shule mvua ikinyesha hawawezi kurudi na wengine wanasombwa na maji ila sasa tunasema asante,” amesema Mwainga.

Mwenge wa Uhuru 2025 umepokelewa wilayani Meatu mkoani Simiyu, ukitokea Wilayani Maswa makabidhiano yaliyofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Vicent Naano kwa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Fauzia Ngatumbura katika kijiji cha Sangaitinje kata ya Itinje Wilayani Meatu, ambao umekagua miradi ya kimaendeleo ya zaidi ya Bilioni 1.97.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *