
Jeshi la Polisi mkoani Singida, limesema chanzo cha ajali ya basi la Ally’s, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda jijini Mwanza na kusababisha vifo vya watu 13 baada kugonga kichwa cha treni katika makutano ya reli na barabara wilayani Manyoni ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa amesema kichwa cha treni kiliacha njia yake na kwenda pembeni mwa reli, na kuwataka madereva wote wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani zinawaongoza ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha TRC, Jamila Mbarouk basi hilo liligonga kichwa cha treni chenye namba V9519006 kilichokuwa kinatokea stesheni ya Aghondi kuelekea Manyoni.
Awali Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Dk Furaha Mwakafwila amesema wamepokea miili ya watu 13 na majeruhi 32.