MWANZA: POLISI WAPIGA MARUFUKU MIKUSANYIKO YA CHADEMA

Jeshi la Polisi katika mkoa wa Mwanza limepiga marufuku mikusanyiko isiyo halali ndani ya mkoa huo kufuatia kuwepo kwa taarifa ya wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA kupanga kukutana na kufanya mikosanyiko isiyo halali kwa lengo la kushinikiza kuachiwa huru kwa mwenyekiti wao Tundu Lissu.

Akizungumza na waandishi wa Habari kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa amesema jeshi la polisi katika mkoa huo limejipanga kikamilifu kufanya doria maeneo yote ya mkoa huo  huku pia akisema wale wote watakaokamatwa kwa ajili ya mikusanyiko hiyo watachukuliwa hatua.

“Kuanzia Aprili 22, 2025 tumeanza kupokea taarifa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali zinazoonyesha kuwa baadhi ya wafuasi wa chama cha Chadema katika Mkoa wa Mwanza wanapanga kukutana na kufanya mikusanyiko isiyokuwa halali kwa lengo la kushinikiza kuachiliwa huru  Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Tundu Lissu ambaye anatarajiwa kufikishwa mahakamani Aprili 24 mwaka huu,” amesema.

“Taarifa zinazopokelewa na Jeshi la Polisi ni kuwa wanawake na watoto wanashawishiwa na baadhi ya viongozi wa chama hicho kushiriki kwa wingi katika mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali,” amesema Kamanda Mutafungwa

Kamanda Mutafungwa amesema kutokana na taarifa hizo jeshi hilo linawatahadharisha wananchi kutojihusisha wala kushiriki katika mikutano hiyo.

“Wale ambao watajihusisha katika mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali au kufanya vurugu, kufanya uvunjifu wowote wa amani Jeshi la Polisi halitasika kuchukua hatua kali za kisheria kama hatua mojawapo muhimu ya kulinda amani na usalama wa Mkoa wa Mwanza,” amesema

Aidha katika hatua nyingine Mutafungwa pia amewaomba wananchi wa mkoa huo kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pale wanapoona mikusanyiko isiyo halali ili jeshi la polisi liweze kufika katika eneo husika na kudhibiti mikusanyiko hiyo.

 “Pia, linawakumbusha wananchi wa mkoa wa Mwanza, kutoa tarifa za mikusanyiko hiyo isiyokuwa halali au uvunjifu wowote wa amani  mara moja itakapojitokeza katika maeneo yao ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa na Jeshi la polisi,”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *