Katika kukabiliana na tatizo la uwepo wa magugu maji katika ziwa Victoria, Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Mwanza wametakiwa kufanya kampeni maalum ya usafi wa mazingira kwenye mialo yote inayozinguka ziwa Victoria ili kutokomeza ukuaji wa magugu maji katika ziwa hilo.
Akitoa maelekezo hayo mapema leo asubuhi Machi 10, 2025 kabla ya kuanza zoezi la kukagua hali halisi ya magugu maji hayo katika eneo la Kigongo Wilayani Misungwi, Luhemeja amebainisha kampeni hiyo ya usafi sasa siyo ya hiari bali ya lazima na kuwataka Wakurugenzi wote wa Halmashauri kuitikia wito huo ili kuepukana na hasara za kuwepo magugu maji hayo ziwani.

“Ndugu zangu hali halisi tunaiona mbele yetu siyo nzuri, hali ya usafiri inazidi kuwa ngumu na ukuaji wa viumbe maji upo hatarini, ni lazima hatua za haraka zianze tukianzia na azimio la usafi”. Amesisitiza Mhandisi Luhemeja
Amesema wamelazimika kuja na Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Maji, na Viongozi wengine waandamizi kutoka Tamisemi na Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka Kanda ya ziwa, lengo ni kukutana na kutoa jawaba la haraka kulinusuru ziwa Victoria na janga hilo.

Awali akiwakaribisha Ofisini kwake viongozi hao waandamizi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema magugu maji yamekuwa tishio katika kukuza uchumi wa buluu kutokana na uwepo wake kunashusha mazalia ya viumbe maji, shida ya usafiri na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba nao kuwa mgumu.
“Nina imani na timu hii iliyochanganyika na wataalamu tofauti na masuala ya mazingira kuja na jawabu chanya ili kuendelea kulipa uhai ziwa Victoria,” Mtanda.
