Na Saulo Stephen – Singida.
Mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mussa Sima wenye thamani ya Shilingi 544,225,626.00 umekamilika na kuzinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Mwang’onda, huku ukitarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa wanafunzi pamoja na kunufaisha wananchi wa Kijiji cha Kinyakaya, Kata ya Unyambwa, Tarafa ya Mungu Maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Mradi huo umetekelezwa kwa mfumo wa Force Account, huku wananchi wakichangia eneo la ujenzi lenye ukubwa wa mita za mraba 43,498 lenye thamani ya Shilingi 47,847,800.00. Ujenzi ulianza Novemba 21, 2024 na kukamilika Aprili 21, 2025, na kwa sasa shule imeanza kutoa huduma za elimu.

Kwa sasa Shule ya Sekondari Mussa Sima ina jumla ya wanafunzi 159, wakiwemo wavulana 61 na wasichana 98. Miundombinu iliyojengwa inajumuisha vyumba nane vya madarasa, maabara tatu za sayansi, jengo la TEHAMA, maktaba, jengo la utawala, ofisi za walimu pamoja na vyoo vya wanafunzi na walimu.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Ndugu Wazo Mwang’onda aliwataka wananchi kuendelea kuutunza mradi huo ili uweze kudumu na kuendelea kutoa huduma bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Alisema uwekezaji huo wa Serikali katika sekta ya elimu utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vyooni, kupunguza utoro, pamoja na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, hatua itakayochangia kuinua kiwango cha elimu katika Manispaa ya Singida.



