Na Saulo Stephen – Singida.
Madiwani, watumishi na wadau wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wametakiwa kuhakikisha kila mmoja anashiriki ipasavyo katika ukusanyaji wa mapato kwa kuzingatia nafasi na majukumu yake, ili Halmashauri hiyo iweze kufikia na kuvuka malengo iliyoweka.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally J. Mwanga, wakati akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo.

Mwanga amesema kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuhakikisha mapato yanakusanywa kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, akisisitiza kuwa ukusanyaji mzuri wa mapato ni muhimu katika kuiwezesha Halmashauri kutekeleza mipango ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesema kila mmoja anapaswa kuwa sehemu ya kuhakikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato yanafikiwa, huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ushirikiano katika kutekeleza majukumu ya Halmashauri.

Aidha, Mwanga amewapongeza madiwani, Mkuu wa Wilaya, watumishi na wadau wa Wilaya ya Ikungi kwa ushirikiano na mshikamano wao katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha Halmashauri inaendelea kutekeleza mipango yake na kufikia malengo yaliyowekwa.


