Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imemhukumu Mwandishi wa Habari, Aloyce Nyanda kulipa fidia ya shilingi bilioni mbili kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, Aron Titus Kagulumjuli, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la udhalilishaji kupitia mitandao ya kijamii.
Hukumu hiyo, imetolewa hii leo na Hakimu Mkazi Bonaventure Lema katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo Buswelu, Wilaya ya Ilemela, ambapo imeelezwa Nyanda kupitia mtandao wake wa kijamii kwa nyakati tofauti alichapisha taarifa za udhalilishaji dhidi ya Aron Kagulumujuli akiwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.
Lema amesema, Mahakama hiyo pia imeweka zuio rasmi kwa Nyanda kutochapisha au kusambaza taarifa yoyote inayomhusu Aron Kagulumjuli au watu wa karibu naye, pamoja na kuondoa taarifa zote zilizopo.

Katika Shauri hilo la madai namba 6166 la mwaka 2024, Kagulumjuli, aliiomba mahakama impe haki dhidi ya kile alichodai kuwa ni mfululizo wa taarifa za kumdhalilisha zilizokuwa zikisambazwa mitandaoni na Nyanda.
Katika shauri hilo, mlalamikaji alikuwa akiwakilishwa na mawakili wake wawili, Godfrey Mlingi na Erick Mutta.
Akizungumza baada ya hukumu, wakili wa mlalamikaji, Erick Mutta, alisema kosa la udhalilishaji kupitia mitandao ya kijamii linakiuka Sheria ya Haki ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2016, chini ya Kanuni ya Nne ya Maadili ya Uandishi wa Habari, kifungu cha 35.
Hata hivyo, wakati hukumu hiyo ikisomwa, Nyanda pamoja na mawakili wake hawakuwepo mahakamani.