Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekuwa anasoma katika shule ya Sekondari Old Shinyanga, Rebeca Maganga (17), ameafriki dunia kwa kujinyonga kwa kutumia mkanda wa sketi ndani ya chumba alichokuwa anaishi.
Akizungumiza tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishina Mwandamizi Msaidizi, SACP. Janeth Magomi amesema tukio limetokea April 27, 2026 majira ya saa saba mchana katika kata ya Old Shinyanga manispaa ya Shinyanga.
Amesema jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga lilipokea taarifa toka kwa mlezi wa marehemu aitwae Peter Mashala ambaye ndiye aliyegundua kifo hicho baada ya kuingia katika chumba cha binti huyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kifo hicho kinahusishwa na msongo wa mawazo baada ya mwananfunzi huyo kurudishwa nyumbani na walimu akitakiwa kurejea shuleni na mzazi kufuatia kutohudhuria masomo kwa muda wa wiki mbili pasipo taarifa yeyote shuleni hapo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kitongoji, Benjamin Andrew amesema walipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa sita machana na kufika katika eneo la tukio ambapo walimkuta mwanafunzi huyo tayari ameshafariki dunia.
Naye mwenyekiti wa jumuiya ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania (SMAUJATA ), Manispaa ya Shinyanga Marystella Nyalusanda ametoa wito kwa wazazi na walezi kujenga tabia ya kuwa karibu na watoto wao.
Amesema ni muhimu familia kuwa na mawasiliano ya karibu ili kubaini mapema changamoto wanazopitia watoto badala ya kuchukua hatua kali kabla ya kutitambua na kulielewa tatizo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya manispaa ya Shinyanga kwa uchunguzi Zaidi, huku jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga likiendelea na uchunguzi Zaidi kuhusiana na tukio hilo.


