Alex lameck (18), mwanafunzi wa shule ya sekondari Tamabu iliyopo katika wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza amepandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya sengerema na kusomewa shtaka la kumjeruhi mwalimu wake kwa kutumia panga.

Alex amesomewa shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 114/2023, ambapo anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 toleo la mwaka 2022.
Akisoma shtaka hilo mbele ya hakimu mkazi mwandamizi, Evod Kisoka, wakili wa serikali, Morice Mtoi amesema mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 25 Septemba 2023 katika shule ya sekondari Tamabu wilayani humo kwa kumjeruhi kwa panga kichwani Stanford Mgaya (37) ambaye ni mwalimu katika shule hiyo kinyume na sheria.
Mshtakiwa amekana shtaka hilo na amedhaminiwa baada ya kutimiza vigezo vya dhamana na shauri hilo limeahirishwa mpaka tarehe 11.10.2023 kwa ajili ya kusoma hoja za awali.