Na Pascal Tuliano – Tabora.
Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha amefanya ziara ya kushtukiza katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora (Tabora Girls) baada ya uwepo taarifa ya mmoja wa Wanafunzi wa Shule hiyo kuwa na ujauzito na kuwa katika mazingira ya shule hiyo mpaka pale alipojifungua na kujaribu kumfunika mtoto huyo kwa ndoo katika moja ya vyoo vya Hospitali ya Rufaa ya Kitete.
Akiwa katika ziara hiyo, RC Chacha amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kumuandikia barua katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera ili kufatilia sababu zilizowafanya wauguzi wa kituo cha afya cha Biharamulo kufanya udanganyifu kwa kujaza (Medical Form) ya kufika nayo kuripoti kidato cha tano ambayo inaonyesha hakuwa na tatizo lolote ili hali akiwa tayari ni Mjamzito.

Pia, amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, kuwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kufatilia swala la Kijana ambaye inasemekana ndiye aliyemlaghai mwanafunzi huyo na kumpa Mimba,
RC Chacha ametoa rai kwa Wananchi wote kuwa serikali ya mkoa haitofumbia macho aina hiyo ya matukio hasa kwa Watoto ambao bado wana ndoto za kusoma.
